Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, hija yake ya kichungaji mjini Sarayevo nchini
Bosnia na Erzegovina, panapo majaliwa hapo tarehe 6 Juni 2015 inalenga kuwaimarisha
Wakristo; kukuza na kukoleza mchakato wa kutafuta mafao ya wengi; kuimarisha udugu,
amani, majadiliano ya kidini na urafiki kati ya watu. Hii ni hija ya tatu ambayo Baba
Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuifanya Barani Ulaya!
Akizungumzia kuhusu
hija hii ya kichungaji ya Baba Mtakatifu huko Sarayevo, Askofu mkuu Luigi Pezzuto,
Balozi wa Vatican nchini Bosnia na Erzegovina anasema kwamba, ni kutokana na kipaumbele
cha pekee kinachotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa maskini na wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa jamii; amana na hazina kuu kwa maisha na utume wa Kanisa. Habari ya
ujio wa Baba Mtakatifu mjini Sarayevo imepokelewa kwa mikoni miwili na kwamba, ni
hija ambayo itachangia kukoleza ustawi na maendeleo ya wananchi wa Bosnia na Erzegovina.
Mji
wa Sarayevo uko njia panda na muhimu sana katika mchakato wa majadiliano ya kidini
na kiekumene, sanjari na majadiliano ya kitamaduni kwani hapa kuna mchanganyiko wa
tamaduni za watu mbali mbali; ili kujenga na kukoleza mchakato wa haki, amani, upatanisho
na umoja wa kitaifa. Baba Mtakatifu anapenda kukutana na Familia ya Mungu sehemu mbali
mbali za dunia, ili kujenga na kukoleza utamaduni wa watu kukutana, ili waweze kuheshimiana
na kuthaminiana, daima akitoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaoishi
pembezoni mwa jamii.
Waamini wanaendelea kuhamasishwa ili kusali kwa ajili
ya kuombea hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko huko Sarayevo, ili kweli iweze
kuzaa matunda yanayokusudiwa katika medani mbali mbali za maisha ya wananchi wa Bosnia
na Erzegovina, lakini zaidi amani na utulivu, upendo na mshikamano, vikolezo vikuu
vya maendeleo.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya
Radio Vatican.