Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano
wa kimataifa mjini Vatican, Jumatatu tarehe 2 Februari 2015 amekutana na kuzungumza
na mabalozi pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican kama mwanzo
wa utume wake. Amewatakia wote ushirikiano, ustawi na maendeleo kwa wote.
Kuwa mwakilishi
wa Vatican sehemu mbali mbali za dunia si utume wa kujivunia, kwani jambo linalopaswa
kupewa kipaumbele cha kwanza ni wito wa Kipadre, kwani amewekwa wakfu kwa ajili ya
kuwagawia Watu wa Mungu Mafumbo ya Kanisa na kuwatangazia Habari Njema ya Wokovu.
Padre au Askofu akiwa na mwelekeo kama huu anaweza kutekeleza dhamana na wajibu wake
kwa moyo mkuu na mnyofu, kwa ajili ya sifa na utuku wa Mungu pamoja na Kanisa.
Ni
maneno ya Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya nchi za nje
na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican katika mahojiano maalum na Radio Vatican,
wakati huu anapojiandaa kutekeleza utume wake mpya hapa mjini Vatican. Alianza shughuli
zake za kidiplomasia nchini Tanzania na kuhitimisha huko nchini Australia.
Askofu
mkuu Gallagher anasema, kwa sasa dunia inakabiliwa na matatizo pamoja na changamoto
kubwa zinazojikita katika mikakati ya maendeleo endelevu inayomgusa mtu mzima: kiroho
na kimwili. Katika shida na mahangaiko yao, watu wanaonesha cheche za matumaini kwa
dunia iliyo bora zaidi, licha ya kinzani, migogoro na vita kuendelea kutikisa misingi
ya maisha ya watu wengi duniani.
Lakini ikumbukwe kwamba, umaskini, ujinga
na maradhi ni matokeo ya vita, uchu wa mali na madaraka pamoja na kutozingatia kanuni
maadili ya kazi. Kwa mwelekeo wa namna hii, watu wanakatishwa tamaa na kujikuta wametumbukia
katika kinzani na migogoro ya kijamii inayoendelea kuhatarisha maisha ya watu wengu
duniani.
Askofu mkuu Gallagher anasema, katika maisha na utume wake kama Mwanadiplomasia
wa Vatican amekutana na upinzani kutoka katika kundi dogo la watu ambao hawatambui
wala kuona mchango wa Vatican na Kanisa katika ustawi na maendeleo ya wengi, lakini
kwa ujumla, Serikali na watu wake wanathamini mchango unaotolewa na Vatican katika
mchakato wa kutafuta mafao ya wengi, kwa kuzingatia kanuni maadili, utu na heshima
ya binadamu. Huu ni mchango wa Kanisa unaobubujika kutoka katika imani, uzoefu na
mang’amuzi ya Kanisa katika historia ya binadamu.
Askofu mkuu Gallagher anasema
kwamba, Marehemu Askofu mkuu Michael Courtney, aliyekuwa Balozi wa Vatican nchini
Burundi na kuuwawa kikatili ataendelea kuwa ni mfano bora katika maisha na utume wake.
Hii inatokana na ukweli kwamba, mara tu baada ya kifo chake, aliteuliwa kwenda kuwa
Balozi wa Vatican nchini Burundi, kunako mwaka 2004. Ni kiongozi aliyejisadaka kwa
ajili ya kujenga msingi wa haki, amani na upatanisho wa kitaifa.
Askofu mkuu
Gallagher anakiri kwamba, katika maisha na utume wake kama Mwanadiplomasia wa Vatican
amesaidiwa na watu mbali mbali aliokutana na kufanya nao kazi katika Balozi mbali
mbali za Vatican na alipokuwa kwenye Sekretarieti ya Vatican. Hapa amekutana na watu
wa kila aina, kila mtu akiwa na malengo, lakini zaidi kwa ajili ya kulitumikia Kanisa.
Kuwa mwanadiplomasia wa Vatican si mali kitu, bali Upadre ndio wito ambao mtu anapaswa
kujivunia na kuhakikisha kwamba, anautunza na kuuendeleza kwa hali na mali.
Na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.