2015-02-03 09:00:57

Familia na maadili!


Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya katika ujumbe wake katika kipindi cha Kwaresima, linawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema nchini humo, kujifunga kibwebwe ili kujenga na kuimarisha familia na taifa kwa kujikita katika utu, kwani mbegu njema zinazopandikizwa kwa wakati hu, zitazaa matunda kwa wakati wake.

Ujumbe wa Kwaresima umetiwa mkwaju na Askofu mkuu Zacchaeus Okoth, Mwenyekiti wa Tume ya haki na amani, Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya. Maaskofu wanasema, familia ni nguzo msingi katika maisha ya jamii ya mwanadamu, ni shule ya ubinadamu na Kanisa dogo la nyumbani. Taifa likifanikiwa kuwa na familia bora na thabiti, taifa litajengeka na kuimarika.

Familia za Kikristo zinachangamotishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, zinajikita katika maisha ya sala, tafakari ya Neno la Mungu, maisha ya Kisakramenti na matendo ya huruma. Familia inayosali na kuwajibika barabara, hiyo itadumu katika mshikamano.

Familia za Kikristo zinahamasishwa na Maaskofu kujitahidi kujisomea Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki ambayo kimsingi ni muhtasari wa Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha Adili na Maisha ya Sala yanayomwilisha katika imani tendaji. Familia zijitajirishe kwa kusoma Maandiko Matakatifu, Maisha ya Watakatifu pamoja na kuendelea kuwarithisha watoto imani na tunu msingi za maisha ya Kikristo na kiutu, kwa njia ya ushuhuda wa mifano bora ya maisha, yenye mvuto na mashiko.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, linawaalika wanandoa watarajiwa kuhakikisha kwamba, wanafanya maandalizi ya kutosha, ili hatimaye, kuweza kugundua na kushiriki kikamimlifu katika maisha ya ndoa na familia, tayari kuwatangazia Watu wa Mataifa Injili ya Familia. Wanandoa watarajiwa wasijikite tu katika maandalizi ya siku ya arusi na kusahau kwamba, kwa njia ya ndoa, wanaanza safari ndefu ya maisha yao yote. Wanandoa watarajiwa walitambue hili na kulizingatia kikamilifu.

Kanisa linawahamasisha Wakristo kuhakikisha kwamba, linawasaidia na kuwasindikiza wanandoa watarajiwa katika maandalizi na baadaye katika hatua mbali mbali za maisha, ili kweli waweze kuwa ni mfano bora wa kuigwa na majirani. Makuzi mema na majiundo makini yaanzie utotoni, kwani mtoto umleavyo ndivyo akuavyo, ili kuwarithisha tunu msingi za maisha ya: Kiroho, Kikristo na Kiutu; kwa kuheshimu na kuwathamini jirani zao sanjari na kuwa na Katekesi makini.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linawaalika waamini kuwasaidia na kuwasindikiza wanandoa wapya, kwani hiki ni kipindi tete sana katika maisha, kwa kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa. Ikumbukwe kwamba, tema inayobeba ujumbe wa Kwaresima kutoka kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya ni: Familia na Maadili.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, Juma la kwanza la Kipindi cha Kwaresima, linawaalika waamini kutafakari kuhusu: Ukabila na Siasa, mambo msingi ambayo yanasababisha changamoto kubwa katika maendeleo na ustawi wa wananchi wengi wa Kenya. Juma la Pili la Kwaresima, waamini watatafakari kuhusu usalama unaopaswa kujionesha katika medani mbali mbali za maisha ya wananchi wa Kenya, tema ambayo kwa hakika inapaswa kuvaliwa njuga kwa kuzingatia kwamba, kwa miezi ya hivi karibuni, wananchi wengi wa Kenya wameguswa na kutikiswa na mashambulizi ya kigaidi; kinzani na migogoro kati ya wakulima na wafugaji.

Juma la nne la Kwaresima, Maaskofu wanawaalika waamini kutafakari kuhusu haki za makundi ya watu wachache na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwani wote hawa ni watoto wa Mungu, wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, wanapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa. Kama sehemu ya Familia ya Kristo, watahukumiwa kwa jinsi walivyowatendea jirani zao.

Juma la tano la Kwaresima, Familia ya Mungu nchini Kenya, itafanya tafakari ya kina kuhusu Serikali na matumizi ya rasilimali ya nchi. Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa na Kanisa kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa kuiongoza nchi, kwa kujikita katika uaminifu, ukweli na uwazi kuanzia ndani ya familia hadi kwenye taasisi za kitaifa.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linakamilisha ujumbe wake wa Kwaresima kwa kuwaalika waamini kufunga kwa ajili ya ukomavu na ukamilifu wa maisha ya Kikristo, ili kuharakisha mchakato wa maisha yanayosimikwa katika utu wema kwa ajili ya familia na taifa kwa ujumla.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.