2015-02-02 07:34:11

Shukrani Kamanda!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumamosi jioni tarehe 31 Januari 2015 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Chuo cha Kipapa cha Wajerumani kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa kumwezesha Kanali Daniel Anrig, mkuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama vya Kipapa kuhitimisha utume wake mjini Vatican na tayari kuanza awamu nyingine ya maisha.

Itakumbukwa kwamba, Kanali Anrig alianza mkataba wake mjini Vatican kunako tarehe 30 Novemba 2008. Vatican inamshukuru na kumpongeza kwa huduma makini aliyoitoa wakati wote alipokuwa Kamanda mkuu wa Vikosi vya wanajeshi kutoka Uswiss, al maarufu kama Swissguards. Ametekeleza dhamana hii kwa kuwajibika, katika hali ya unyofu, uaminifu na ushirikiano mkuu na wadau mbalimbali katika vikosi vya ulinzi na usalama mjini Vatican. Amekabiliana na matatizo, changamoto na fursa mbali mbali, lakini akatoa majibu makini yaliyojikita katika imani na tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu, daima akitegemea tunza na ulinzi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Katika mahubiri yake, Kardinali Parolin amewataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kujitaabisha kumfahamu Yesu Kristo, ili hatimaye, kujenga mahusiano ya kweli na mema, ili kufahamu na hatimaye, kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao. Yesu aliosha madaraka katika kufundisha na kutenda kama sehemu ya utekelezaji wa utume na wajibu wake. Hakukata tamaa alipokutana na magumu na hata kutakiwa kutoa maamuzi machungu katika maisha. Alifahamu mahitaji ya wasikilizaji wake na kuwafunda kadiri ya mapenzi ya Mungu.

Yesu Kristo, Masiha na Mkombozi, alikuja duniani ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, kwa njia ya Fumbo la Msalaba, akaonesha ushindi dhidi ya shetani kwa kufufuka kutoka katika wafu, changamoto kwa waamini kujenga na kudumisha mahusiano ya kweli na dhati na Kristo Yesu.

Kardinali Parolin anawaalika waamini kujiuliza kuhusu mahusiano yao na Yesu Kristo, ikiwa kama kweli wamemkubali kama Mwana wa Mungu aliyekuja kuwakomboa au wamebaki wakipigwa na bumbuwazi kutokana na miujiza aliyokuwa anatenda, bila kumpatia nafasi ya kuingia katika maisha na mioyo yao?

Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya Nne ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa inamwonesha Yesu anyefundisha na kutenda kwa mamlaka, kielelezo makini kitakachopata utimilifu wake pale juu Msalabani. Kanisa linawashukuru kwa namna ya pekee wanajeshi kutoka Uswiss ambao wamekuwa wakijisadaka kwa ajili ya ulinzi na usalama wa Baba Mtakatifu mjini Vatican, utume wanaoutekeleza kwa imani na sadaka kubwa ya maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.