Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujadili na kuibua mbinu mkakati inayoweza kutumika
kwa ajili ya kung’oa ukatili unaofanywa dhidi ya wasichana na wanawake katika mapambano
ya silaha sehemu mbali mbali za dunia; hali ambayo kwa sasa inazidi kushamiri kwa
kasi ya ajabu.
Wasichana na wanawake ndio waathirika wakuu katika mapambano
ya silaha, kutokana na mfumo dume ambao bado unaathari kubwa katika kulinda na kutetea
haki msingi za wanawake na wasichana duniani. Unyama na ukatili huu unajionesha kwa
namna ya pekee katika nyanyaso za kijinsia, utumwa wa ngono sanjari na biashara haramu
ya binadamu, mambo ambayo ni kinyume cha utu na heshima ya binadamu kadiri ya Mafundisho
Jamii ya Kanisa.
Kanisa linaamini na kufundisha kwamba, binadamu wote ni sawa
kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu, wana utu na heshima inayopaswa
kulindwa na kudumishwa, kumbe, nyanyaso dhidi ya binadamu ni kinyume kabisa cha utu
na heshima yake. Huu ni mchango uliotolewa na Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye
Umoja wa Mataifa na kusomwa kwa niaba yake na Monsinyo Janusz Urbanczyk kwenye Baraza
la Usalama la Umoja wa Mataifa, katika kikao chake kilichohitimishwa hivi karibuni
mjini New York, Marekani. Nyanyaso za kijinsia ni mambo ambayo yanaacha madhara ya
kudumu kwa waathirika.
Ujumbe wa Vatican unakazia kwamba, vita ni kati ya mambo
ambayo yanaathari kubwa katika mchakato wa ulinzi na usalama wa jamii husika na kwamba,
familia zinaathirika vibaya zaidi, kwani mara nyingi watu wanalazimika kuyakimbia
makazi yao, hali inayopelekea familia kusambaratika na hatimaye, kunyonywa zinapokuwa
ugenini. Bila ulinzi wa kutosha, haki msingi za binadamu zitaendelea kuwekwa rehani
chini ya mtandao wa vitendo vya kigaidi.
Inasikitisha kuona kwamba, Jumuiya
ya Kimataifa inashindwa kutoa ulinzi wa kutosha kwa wanawake na wasichana kutokana
na imani yao, hali ambayo inatishia amani na usalama wa Wakristo katika baadhi ya
maeneo duniani. Hapa kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa, Serikali husika na viongozi
wa kidini kulaani vikali mashambulizi yanayofanywa kwa misingi ya kidini.
Baba
Mtakatifu Francisko, anaendelea kusema kwamba, biashara haramu ya binadamu inazidi
kukua na kushamiri, jambo ambalo ni uhalifu dhidi ya ubinadamu. Hapa kuna haja kwa
Jumuiya ya Kimataifa kujifunga kibwebwe ili kuhakikisha kwamba, biashara haramu ya
binadamu inakomeshwa, kwani inagusa utu na heshima ya binadamu.
Kanisa Katoliki
kwa njia ya Mashirika na Taasisi zake, litaendelea kutoa msaada wa hali na mali kwa
waathirika wa biashara haramu ya binadamu pamoja na kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa,
ili kukomesha biashara hii. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kukata katu katu utamaduni
wa utumwa mamboleo, kwa kujielekeza zaidi katika ujenzi wa amani kwa kujikita katika
Injili ya Uhai sanjari na kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa na Serikali husika
zinatekeleza dhamana na wajibu wake barabara.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.