2015-02-02 07:39:06

Majadiliano ya kidini


Jumuiya ya Kimataifa kuanzia tarehe 1 hadi tarehe 7 Februari 2015 inaadhimisha Juma la kimataifa la maridhiano na majadiliano ya kidini kati ya dini mbali mbali duniani, lililoanzishwa na Umoja wa Mataifa kunako mwaka 2010. Hii ni fursa kwa viongozi mbali mbali wa kidini katika nyumba za Ibada kusaidia mchakato wa kufundisha umuhimu wa waamini kuheshimiana na kuvumiliana; kupendana na kusaidiana pamoja na kushikamana kwa ajili ya mafao na ustawi wa wengi.

Changamoto hii ina umuhimu wa pekee kwa nyakati hizi, ambamo kuna kinzani na migogoro mingi ya kidini inayofuka moshi, kiasi hata cha kutishia usalama, amani na ustawi na mendeleo ya wengi. Viongozi wa dini na waamini katika ujumla wao, wanapaswa kuwa ni vyombo vya haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati kati ya watu na kamwe wasitumie dini kuwa ni chanzo cha vita na migawanyiko ya kijamii.

Viongozi wa kidini wanapaswa kuwasaidia wafungwa ili kufanya mabadiliko ya kina katika maisha yao wanapomaliza kutumikia adhabu, tayari kuanza ukurasa mpya wa maisha uraiani. Vijana wasaidiwe kuwa kweli ni vyombo vya haki na amani na kamwe wasitumiwe kuwa ni vyanzo vya machafuko na vita, kama inavyojionesha sehemu mbali mbali za dunia.

Kimsingi, viongozi wa dini na waamini mbali mbali wanachangamotishwa na Umoja wa Mataifa kuwa kweli ni vyombo vya upendo, haki, amani na maridhiano kati ya watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.