Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu ni kati ya wajumbe
wakuu watakaoshiriki kwenye Kongamano kuhusu Familia litakalofanyika kwenye Kanisa
kuu la Kupashwa Bwana Habari, mjini Nazareth, Jumamosi tarehe 7 Februari, 2015. Kongamano
hili linaongozwa na kauli mbiu "Wito na utume wa Familia ndani ya Kanisa na Ulimwengu
mamboleo".
Kardinali Baldisseri ataratibu maoni, mawazo, tafakari na tafiti
mbali mbali zitakazowasilishwa na wajumbe kama sehemu ya mchango wao wa maandalizi
ya hati ya kutendea kazi kwa ajili ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia
itakayofanyika mwezi Oktoba hapa mjini Vatican. Viongozi wakuu kutoka Nchi Takatifu
wanatarajiwa kushirikisha mawazo na mang'amuzi yao.
Kardinali Baldisseri atakapowasili
Nchi Takatifu, Ijumaa tarehe 6 Februari anatarajiwa kukutana na familia, kubariki
na hatimaye, kuzindua nyumba mpya ya mapokezi kwa ajili ya familia ambazo zinafanya
hija ya maisha ya kiroho kwenye maeneo matakatifu. Kardinali Baldisseri wakati wa
kongamano, atawashirikisha wajumbe hatua ambazo zimekwishafikiwa katika mchakato wa
maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia. Jumapili, ataadhimisha Ibada ya
Misa kwa kutoa Daraja la Ushemasi na Upadre kwa baadhi ya watawa wanaoishi huko Nchi
Takatifu.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio
Vatican.