2015-02-02 08:22:47

Funga domo lako!


Huyu ni nani? Kuanzia jumapili hii na nyingine 12 zifuatazo, Neno la Mungu litajikita katika swali hili. Jibu la swali hili tutalipata katika Jumapili ya 24 ambapo Injili ya Marko inatoa jibu kwa swali hili. Nii katika ufunuo ule wa askari wa kirumi tunapata jibu – Mk. 15:39 – akida aliyesimama mbele yake, alipoona jinsi alivyokata roho alisema, hakika, mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu. Yesu – anaingia katika Sinagogi. Kila Sabato walikuwa wanapata mafundisho, lakini leo fundisho lake ni tofauti – aliwafundisha kama mtu mwenye mamlaka – Mk. 1:22 maana yake nini kufundisha kwa mamlaka?

Tukilinganisha mafundisho ya Yesu na walimu wa Sheria twaona tofauti kubwa tatu (3).Tofauti kubwa ya kwanza ipo katika chanzo cha fundisho lenyewe, yaani fundisho linatoka wapi. Fundisho la Yesu ni: Fundisho lilitoka moyoni na si kichwani.Lina mwelekeo wa roho mpya na si sheria tu.

Ni changamoto ya kuwa tayari kuanza upya. Mafundisho ya Yesu yamejaa uhakika kwa vile anajua anaongea ukweli wenye uzima – angalia Yn. 3: 11 – amin, amin, nakuambia, twasema tunayoyajua, twashuhudia tuliyoyaona, lakini hampokei ushuhudu wetu. Mafundisho yake ni ushuhuda wa uhusiano wake na Mungu. Walimu wa Sheria, chanzo cha mafundisho yao ni sheria.


Tofauti kubwa ya pili kubwa kati ya mafundisho ya Yesu na yale ya walimu wa Sheria ipo katika maana ya fundisho lenyewe. Yesu anaangalia thamani ya Sheria na maana yake. Waandishi wa Sheria wanakazia ufafanuzi wa maneno – m.f. kuhusu sabato – lini sabato yaanza na lini inaisha na kazi ipi ya kufanya na ipi siyo.
Yesu anaelezea mpango kazi wa Mungu. Maana mpya ya Sabato ni kujiacha kwa ajili ya Mungu ili kufanya kazi ya Mungu – Yn. 5:17 - Yesu akasema, Baba yangu anaendelea na kazi yake, nami ninafanya vivyo hivyo. Yesu anaponya, siku ya sabato. Kwa Wayahudi ikawa ni dhambi ya mauti. Sasa kati ya kuacha mgonjwa aendelee kuteseka, kushika sabato kwa sababu sheria inasema hivyo na kumponya mgonjwa ni ipi ina maana zaidi?

Hii ndiyo taarifa ya ukombozi ya Kristo, taarifa inayokomboa. Tofauti nyingine ipo katika ujumbe wenyewe:Ujumbe wa Kristo watualika kubadilika moyoni. Ujumbe wa walimu wa sheria – wafanya watu wajisikie vibaya, inatisha, kuogofya. Yesu alipopelekewa yule kipofu – alimponya. Walimu wa sheria – nani aliyetenda dhambi. Yesu anafundisha na kutibu.Wayahudi wanalaumu na kuona kakufuru.


Ndugu zangu, huu mtazamo mpya wa Kristo uwe leo changamoto kubwa katika maisha yetu. Ni vizuri pia tukatumia neno la Mungu siku ya leo kuangalia maisha yetu ya ufuasi. Ni vizuri kuangalia sheria zetu na sheria au amri za Mungu na kuona tuko wapi au tukoje. Kama Kristo alivyofanya, tukumbuke kuwa jukumu la kwanza ni kumkomboa mwanadamu na hali yake mbaya. Hatuna budi kuweka katika matendo kile ambacho tunakiamini katika imani yetu kama Kristo alivyofanya na alivyotufundisha kuishi.

Masomo yetu ya leo yanatuita tuiitikie sauti ya Mungu. Katika somo la kwanza – tunaona jinsi mwandishi anavyotambua mapenzi ya Mungu. Mungu anaahidi Nabii, mtu mpole, msemaji mwaminifu wa neno, mtu wa imani na mlinzi wa huruma ya Mungu. Ndiyo sisi leo. Sote tunatakiwa kuwa huyo nabii wa Mungu katika mazingira yetu ya leo. Katika somo la Injili tunaona kuwa, alipo Yesu, upo ufalme wa wake na wa Baba yake. Hivyo shetani hana nguvu tena. Uwepo wa Kristo ni uzima mpya na wa milele.

Tumsifu Yesu Kristo.

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.