2015-01-31 11:11:41

Yatakayojiri Februari - Aprili 2014


Ratiba elekezi ya maadhimisho mbali mbali yatakayofanywa na Baba Mtakatifu Francisko kwa mwezi Februari hadi Aprili 2015 inaonesha kwamba, matukio makuu kwa wakati huu ni pamoja na kuwasimika na kusali na Makardinali wapya 20 walioteuliwa hivi karibuni. RealAudioMP3

Ibada ya jumatano ya Majivu, mwanzo wa Kipindi cha Kwaresima, muda wa toba na wongofu wa ndani unaojikita katika utandawazi wa mshikamano wa mapendo; mafungo ya kiroho, huko Ariccia ili kujichotea nguvu. Hija ya kichungaji huko Pompei, Napoli, Kusini mwa Italia pamoja na Ibada za Juma kuu zitakazokamilishwa kwa Siku kuu ya Pasaka.

Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 2 Februari 2015, Siku kuu ya kutolewa Bwana Hekaluni, anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kuanzia majira ya saa 11: 30 saa za Ulaya, kwa ajili ya watawa kama sehemu ya maadhimisho ya siku ya 19 ya Watawa Duniani, sanjari na Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani.

Tarehe 8 Februari, Jumapili ya Tano ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa, Baba Mtakatifu atatembelea Parokia ya “San Michele Arcangelo, iliyoko Pietralata, Jimbo kuu la Roma, kuanzia majira ya saa 10: 00 jioni. Tarehe 14 Februari 2015, majira ya saa 5: 00 asubuhi, Baba Mtakatifu katika Kanisa kuu la Mtakatifu Petro atawasimika rasmi Makardinali wapya 20 walioteuliwa hivi karibuni sanjari na kupembua majina ya wenyeheri kadhaa watakaoandikwa na Mama Kanisa katika orodha ya Watakatifu. Jumapili, tarehe 15 Februari 2015, majira ya saa 4: 00, Baba Mtakatifu ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na Makardinali wapya, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Tarehe 18 Februari, Jumatano ya Majivu, Baba Mtakatifu atakianza kipindi cha Kwaresima kwa maandamano ya toba na baadaye Ibada ya Misa takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Anselmi, lililoko mjini Roma kuanzia saa 10: 30 Jioni. Jumapili tarehe 22 Februari 2015, Baba Mtakatifu pamoja na wasaidizi wake wa karibu wataondoka kwenda Ariccia “kujichimbia huko” kwa ajili ya mafungo ya kiroho hadi Ijumaa, tarehe 27 Februari 2015.

Tarehe 8 Machi 2015, Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Kwaresima, Baba Mtakatifu Francisko, majira ya jioni kuanzia saa 10: 00 atatembelea na kusali na waamini wa Parokia ya “Santa Maria Madre del Redentore; iliyoko Tor Bella Monaca, Jimbo kuu la Roma. Baba Mtakatifu Francisko ataongoza Ibada ya toba kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Ijumaa tarehe 13 Machi 2015, kuanzia saa 11:00 jioni. Baba Mtakatifu atatembelea Jimbo kuu la Napoli na kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Pompei. Papa ataufunga mwezi Machi kwa maadhimisho ya Jumapili ya Matawi, mwanzo wa Juma kuu hapo tarehe 29 Machi 2015, Ibada ya Misa na maandamano yataanza majira ya saa 3: 30, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Mwezi Aprili, Alhamisi kuu, Baba Mtakatifu ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kubariki Mafuta Matakatifu; Ijumaa kuu, ataongoza Ibada ya Mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo, Jumamosi kuu, ataongoza mkesha wa Pasaka na Siku kuu ya Pasaka, kuanzia saa 4:15 ataongoza Ibada ya Misa Takatifu na baadaye kutoa baraka kwa mji wa Roma na Dunia kama zinavyojulikana kwa lugha ya Kilatini “Urbi et Orbi”. Na jumapili ya Huruma ya Mungu, hapo tarehe 12 Aprili 2015, Baba Mtakatifu anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya waamini wanaotumia madhehebu ya Kiarmeni.

Kama kawaida, Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican itaendelea kukujuza yale yatakayokuwa yanajiri katika maadhimisho haya, lakini kwa wale wenye haraka wanaweza kutembelea kwenye mtandao wetu: Chungulia lugha ya Kiswahili, hapo utakuwa umefika!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.