2015-01-31 14:43:58

Utu na heshima ya binadamu!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumamosi, tarehe 31 Januari 2015 katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya Mtakatifu Yohane Bosco, miaka mia mbili tangu alipozaliwa; Mtakatifu aliyejisadaka kwa ajili ya huduma ya kichungaji na elimu kwa vijana, amezindua rasmi mwaka wa shughuli za mahakama ya mji wa Vatican kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Mtakatifu Yohane Bosco katika mbinu zake za malezi kwa vijana, alijikita zaidi katika kuzuia, kuunda na kushawishi, akiwaachia vijana kujiweka wazi mbele ya Mwenyezi Mungu, ili aweze kuwafunda zaidi. Ni mtakatifu ambaye alichota mambo mengi ya maisha na utume wake kutoka kwa Mtakatifu Francisko wa Sale, akionesha utu, heshima, wajibu na haki ya kila mtu inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Baba wa wote. Imani kwa Kristo na Kanisa lake, imekuwa ni chachu ya mabadiliko kwa watu wengi duniani.

Mwaka wa shughuli za mahakama ni sehemu ya mchakato wa huduma ya ukweli inayojikita katika mchakato wa elimu, dhamana inayotekelezwa katika shughuli za mahakama zinazopaswa pia kuwa na mwono wa kiimani kwani sheria ni kwa ajili ya kumsaidia mwanadamu kutenda mema ili kufikia uzuri; watu wajenge utamaduni wa kuzingatia utawala wa sheria; haki msingi za binadamu sanjari na haki jamii, huku wakiongozwa na kanuni ya dhahabu.

Watu wapewe elimu ya kujizuia kutenda mabaya, kwa kujenga utamaduni wa kusikiliza, majadiliano pamoja na kutakiana mema, ili kujenga raia wema na wenye kuwajibika, watu wanaopenda na kuheshimu sheria na kutenda haki, bila kujitumbukiza katika hatari ya kutaka kulipiza kisasi. Ni wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inatambua kwanza: utu na heshima ya binadamu.

Lengo la shughuli za mahakama zinazotekelezwa mjini Vatican ni kwa ajili ya afya ya mioyo ya waamini inayojikita katika sheria asilia, sheria za Kanisa pamoja na Injili, yote haya ni kwa ajili ya mafao ya wengi, anasema Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.