Katika hali ya kuchoka na kukata tamaa baada ya kuvua samaki usiku kucha, Yesu aliwatokea
mitume wake akawaambia kushusha nyavu zao, kwa imani na matumaini, Petro akamwambia
Yesu, kwa neno lako, tutazishusha nyavu zetu na hapo, wakashangaa kwa wingi wa samaki
waliopata.
Huu ndio ujumbe wa matumaini unaotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki
Sudan ya Kusini baada ya mateso na masumbuko ya vita ya wenyewe kwa wenyewe, sasa
wanaitaka Familia ya Mungu nchini Sudan ya Kusini kujikita katika mchakato wa kujenga
na kudumisha: haki, amani, umoja na upatanisho wa kitaifa na kwamba, hakuna tena sababu
msingi ya kuhalalisha vita na kwamba, inapaswa kukomeshwa mara moja!
Baraza
la Maaskofu Katoliki Sudan ya Kusini, linawaalika viongozi wa kisiasa kuanza kujikita
katika majadiliano ya kina, ili kusaidia mchakato wa kupata suluhu ya kudumu, kwa
kuthubutu kwenda mbali zaidi, licha ya jitihada ambazo pengine hapo awali hazikuweza
kuzaa matunda yanayokusudiwa, ili kurejesha tena misingi ya haki, amani na utulivu
na kwamba, Maaskofu wanapenda kuwaunga mkono kwa jambo hili.
Vita inapaswa
kusitishwa mara moja, vinginevyo, Sudan ya Kusini itabaki kuwa ni makaburi tupu na
hatimaye kutoweka katika ramani ya dunia kwani vita ni uovu na kinyume cha mapenzi
ya Mungu. Watu waoneshe ujasiri wa kusema kwamba, vita ni dhambi bila kupindisha maneno.
Vita haiwezi kuwa ni sababu ya majadiliano ya kila siku huko Addis Ababa, wakati watu
wanapoteza maisha nchini Sudan ya Kusini. Hakuna ushindi wa kisiasa unaopatikana kwa
njia ya mauaji ya watu wasiokuwa na hatia, Kanisa kama Mama na Mwalimu, linaomboleza
kwa vifo vya watoto wake wote bila ubaguzi.
Chanzo kikubwa cha vita, kinzani
na migogoro ya kijamii ni uchu wa mali na madaraka pamoja na tabia ya kutaka kulipizana
kisasi, taifa la Sudan ya Kusini linapaswa kuepushwa na majanga kama haya ambayo hayana
mvuto wala mashiko kwa ustawi na maendeleo ya watu, wanasiasa watambue kwamba, uongozi
ni huduma inayopania kukoleza: haki na amani; maendeleo na ustawi wa raia wake wote
kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mafao ya wengi.
Mpasuko uliojitokeza Sudan
ya Kusini tangu mwaka 2005 hadi mwaka 2013 ni matokeo ya: rushwa na ufisadi; ukabila
na upendeleo; ukosefu wa sera na mikakati madhubuti ya maendeleo; udhaifu katika kurekebisha
mfumo wa vikosi vya ulinzi na usalama. Umefika wakati badala yakutumia fedha kununulia
silaha, fedha hizo sasa zielekezwe katika ujenzi wa miundo mbinu pamoja na kuimarisha
demokrasia ya kweli kwa kutekeleza kwa matendo mkataba wa amani uliofikiwa mjini Arusha,
Tanzania mwanzoni mwa mwezi Januari.
Uchaguzi mkuu unaweza kufanyika Juni 2015,
lakini utawala wa sheria na Katiba ya nchi ni mambo msingi ya kuzingatiwa, kumbe,
kuna haja kwa wadau mbali mbali kushirikiana kwa pamoja katika kipindi hiki cha mpito,
hadi mazingira yatakaporuhusu kufanyika kwa uchaguzi mkuu. Ukwapuaji wa maeneo makubwa
ya ardhi, migogoro ya ardhi; kinzani kati ya wakulima na wafugaji ni mambo yanayopaswa
kushughulikiwa kikamilifu, ili kulinda na kudumisha amani na utulivu.
Baraza
la Maaskofu Katoliki Sudan ya Kusini linaonya kwamba, kuna idadi kubwa ya silaha za
kisasa zinazomilikiwa na raia kinyume cha sheria, jambo ambalo linaweza kuhatarisha
amani na usalama wa raia na mali zao. Maaskofu wanawataka wananchi kujikita katika
utawala wa sheria. Kanisa Katoliki litaendelea kushirikiana na Baraza la Makanisa
Sudan ya Kusini katika mchakato wa kujenga msingi wa haki, amani na upatanisho wa
kitaifa.
Baraza la Maaskofu Katoliki linawaaalika waamini na watu wote wenye
mapenzi mema kutafakari kwa kina na mapana ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika
kipindi cha Kwaresima kwa mwaka huu, kwa kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa
na mahangaiko ya jirani na badala yake, kujenga na kudumisha mshikamano wa upendo,
udugu na umoja kati ya watu, tayari kujikita katika mchakato amani na upatanisho wa
kitaifa.
Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan ya Kusini linahitimisha ujumbe wake
wa matumaini kwa kuwataka wananchi wa Sudan ya Kusini kuachana kabisa na vita na badala
yake kushirikiana kwa pamoja katika mchakato wa ujenzi, ustawi na maendeleo ya wananchi
wote.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.