Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI limehitimisha mkutano wake wa mwanzo wa mwaka
kwa kukazia umuhimu wa kuibua mikakati itakayowawezesha vijana kupata fursa za ajira,
ili kuweza kuwa na matumaini ya kesho iliyo bora zaidi.
Maaskofu wanakazia
na kuendelea kuhimiza waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujenga na kudumisha
tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu
sanjari na kukataa utamaduni wa kifo na utandawazi usioguswa na shida pamoja na mahangaiko
ya wengine.
Maaskofu wanasema, wataendelea kujadiliana na wadau mbali mbali,
ili kuhakikisha kwamba, mafao ya wengi yanapewa kipaumbele cha kwanza. Wamejiwekea
mikakati ya utekelezaji wa Waraka wa kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko, Injili
ya Furaha, Evangelii gaudium katika maisha na utume wa Kanisa nchini Italia. Wanaendelea
kukazia maisha na utume wa Wakleri sanjari na majiundo yao ya awali na endelevu, ili
kujenga na kudumisha umoja na mshikamano kati ya Familia ya Mungu.
Ufafanuzi
huu umetolewa na Askofu Nunzio Galantino, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki
Italia alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari mjini Roma, Ijumaa tarehe 30 Januari
2015. Anasema, Kongamano la kikanisa kitaifa litakalofanyika Jimbo kuu la Firenze
kuanzia tarehe 9 hadi tarehe 13 Novemba 2015 litaweka dira na mkakati wa maisha na
shughuli za kichungaji nchini Italia katika kipindi cha miaka kumi ijayo, kwa kutoa
kipaumbele cha pekee kwa Kanisa linalowajali na kuwahudumia maskini; mafao ya wengi
pamoja na ujenzi wa utamaduni wa upendo na mshikamano.
Na Padre Richard A.
Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.