2015-01-31 14:49:14

Someni alama za nyakati!


Katika maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani ni changamoto kwa watawa wa Mashirika mbali mbali kuhakikisha kwamba, wanajisadaka bila ya kujibakiza katika utoaji wa huduma, kwa kusoma alama za nyakati, ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo. Watawa wanapaswa kuwa ni mashuhuda hai wa furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake, kwa kutambua kwamba, Yesu Kristo ni chemchemi ya furaha ya kweli katika maisha yao na kamwe, hawawezi kupta furaha ya kweli kwa kumezwa na malimwengu au kwa kupenda mno utajiri na mali!

Hii ni changamoto inayotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Canada katika maadhimisho ya Siku kuu ya kutolewa Bwana Hekaluni ambayo kimsingi pia ni Siku ya Watawa Duniani, ambayo kwa mwaka huu inakwenda sanjari na maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani.

Watawa wanachangamotishwa kuwa kweli ni manabii, kwa kujitahidi kumwilisha tunu msingi za maisha ya Kiinjili katika uhalisia wa maisha yao, ili kujenga udugu, ukarimu na upendo wa dhati. Ni wajibu wa watawa kuhakikisha kwamba, wanadumisha umoja na mshikamano, kielelezo cha neema ya Mungu inayotenda kazi ndani mwao.

Watawa wawe tayari kujisadaka katika mchakato wa Uinjilishaji mpya kwa kuwaendea maskini na wote wanaoishi pembezoni mwa jamii; ili kuwahudumia na kuwafariji: wakimbizi, wahamiaji pamoja na kuwamegea katekesi ya kina; mambo ambayo kwanza kabisa hayana budi kupata chimbuko lake katika tafakari ya Neno la Mungu, maisha ya Sala na Sakramenti za Kanisa; wakiwa daima tayari kutafuta na kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha na utume wao. Watawa kwa njia ya karama za mashirika yao wanaweza kusaidia mchakato wa Uinjilishaji mpya, tayari kupambana na changamoto za Uinjilishaji, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linawataka watawa kuangalia historia ya waanzilishi wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume kutoka nchini humo, kwa kuwa na ujasiri wa kufanya marekebisho makubwa, tayari kutoka kifua mbele kuwatangazia watu Injili ya Furaha, kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Maaskofu wanawapongeza na kuwashukuru watawa kwa kushikamana na maskini pamoja na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii na kwamba, huduma yao ina umuhimu wa pekee katika maisha na utume wa Kanisa nchini Canada.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.