Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi, limehitimisha mkutano wake wa mwanzo wa mwaka
kwa kuchambua kwa kina na mapana athari za mafuriko yaliyosababisha maafa makubwa
kwa wananchi wa Malawi; utekelezaji wa maazimio ya mkutano mkuu wa kumi na nane wa
AMECEA uliofanyika nchini Malawi kunako mwaka 2014; tathmini ya hija ya kitume ya
Baraza la Maaskofu Katoliki mjini Vatican; hali halisi ya kisiasa na kiuchumi nchini
Malawi.
Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi limeangalia kwa uchungu mkubwa maafa
yaliyosababishwa na mafuriko ambayo hayajawahi kutokea nchini humo na kusababisha
watu zaidi ya elfu mbili kupoteza maisha na wilaya kumi na tano kuathirika vibaya.
Maaskofu wamejiwekea mikakati ya kuratibu misaada ya dharura kwa ajili ya kuwasaidia
wananchi walioathirika kutokana na mafuriko hayo ili waweze kuanza tena upya kwa imani
na matumaini.
Maaskofu wamejadili pia maazimio yaliyopitishwa na Shirikisho
la Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, ili kukabiliana na
changamoto za Uinjilishaji unaojikita katika wongofu na ushuhuda wa imani kwa Kristo
na Kanisa lake. Wameangalia kwa kina na mapana tunu msingi za maisha ya ndoa na familia,
changamoto na fursa zilizopo, ili kuliwezesha Kanisa kuendelea kutangaza Injili ya
Familia kwa ari na moyo mkuu bila kusahau umuhimu wa ujenzi wa amani.
Maaskofu
wanasema, kuna haja kwa Kanisa nchini Malawi, kuendelea kujielekeza katika Uinjilishaji
wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; kwa kuwa na mbinu mkakati
wa Uinjilishaji unaowasaidia waamini kupata katekesi makini na endelevu; ili kuwajengea
moyo wa toba na wongofu wa ndani; tayari kumshuhudia Kristo kwa njia ya imani tendaji
katika medani mbali mbali za maisha.
Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi limetathmini
hija ya kitume lililoifanya mjini Vatican kuanzia tarehe 5 hadi tarehe 12 Novemba
2014; wakaangalia pia hali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii pamoja na kufanya tathmini
ya kina kuhusu uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Malawi mwaka 2014. Baraza la Maaskofu
limepitisha pia Katiba ya Chama cha Kitume cha Uamsho wa Kikatoliki pamoja na Umoja
wa Wanawake Wakatoliki wa Malawi.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.