Umoja wa Afrika katika mkutano wake uliokuwa unafanyika mjini Addis Ababa, umepitisha
mkakati wa kuunda kikosi maalum cha kupambana na kikundi cha Boko Haram ambacho kimekuwa
ni tishio kwa amani na usalama huko Nigeria na katika nchi jirani na kwamba, hatua
ya pili kwa sasa ni kuomba kibali kutoka katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Ikiwa kama mpango huu utakubaliwa, ina maana kwamba, Umoja wa Mataifa utasaidia
kuchangia gharama za kupambana na kikosi cha kigaidi cha Boko Haram, huko Kaskazini
mwa Afrika na kwamba, operesheni hii itaratibiwa mjini N'Djamena, nchini Chad.Tangu
Cameroon, Chad na Nigeria zilipoamua kuunganisha nguvu zao dhidi ya kikundi cha kigaidi
cha Boko Haram, wachunguzi wa mambo wanasema, kumeanza kuonekana dalili za mafanikio.
Uamuzi
wa kuunda kikosi kazi ili kupambana na Boko Haram umefikiwa katika mkutano wa baadhi
ya Marais kutoka Afrika Magharibi uliokuwa unaratibiwa na Bibi Nkosazana Dlamin Zuma,
Kamisheni wa Umoja wa Afrika, aliyekiri kwamba, vitendo vya kigaidi hasa vile vinavyofanywa
na Boko Haram vinatishia amani, usalama, ustawi na maendeleo ya Bara la Afrika. Ameitaka
Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inasaidia kutoa jibu makini na lenye uhakika
katika mapambano dhidi ya Boko Haram.
Umoja wa Afrika umejadili pia mbinu mkakati
ya kupambana na ugonjwa wa Ebola ambao kwa kipindi cha mwaka mmoja, umesababisha maafa
makubwa kwa maisha na maendeleo ya watu wengi huko Afrika Magharibi, ingawa kwa sasa
maambukizi kadiri ya taarifa ya Shirika la Afya Duniani yanaendelea kupungua, lakini
bado Ebola ni tishio kwa usalama na maisha ya watu wengi.