2015-01-30 11:13:34

Watawa asanteni sana!


Katika maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, Baraza la Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika, linalounganisha Maaskofu kutoka Botswana, Swaziland na Afrika ya Kusini, linawapongeza na kuwashukuru Watawa wa mashirika mbali mbali waliojisadaka kwa ajili kuanzisha Makanisa mahalia, wakahudumia kwa moyo wa upendo na majitoleo makuu parokia sanjari na kutoa huduma iliyotukuka katika sekta mbali mbali za maisha ya mwanadamu!

Shukrani hizi zimo katika barua ya kichungaji iliyoandikwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika wakati huu, Mama Kanisa anapoendelea kuadhimisha Mwaka wa Watawa uliotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko. Kwa namna ya pekee, Maaskofu wanawakumbuka watawa wote ambao wametangulia mbele ya haki, wakiwa na matumaini ya ufufuko na maisha ya uzima wa milele. Baadhi yao wamezikwa katika makaburi yasiyokuwa na alama wala kielelezo, lakini hazina ya imani waliyoitangaza bado imehifadhiwa katika sakafu ya mioyo ya Familia ya Mungu, Kusini mwa Afrika.

Maaskofu wanawapongeza na kuwashukuru watawa ambao wameamua kumalizia maisha yao wakiwa na Familia ya Mungu Kusini mwa Afrika na kwamba, ushuhuda na ujasiri wao utaendelea kukumbukwa na wengi. Maaskofu wanawakumbuka na kuwaombea watawa walionea sehemu mbali mbali za dunia, ambao wanaendelea kujisadaka kwa ajili ya mchakato wa Uinjilishaji mpya na ule wa kina, ili kuwaonjesha watu Injili ya Furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.

Watawa wote hawa wanaendelea kushuhudia huduma ya kimataifa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu, Kusini mwa Afrika, changamoto ya kuachana na ubaguzi wa rangi unaoweza kuhatarisha amani, upendo na mfungamano wa kijamii kati ya watu. Kuna haja ya kusaidiana na kutaabikiana, kwa kuvuka kishawishi cha ukabila na tamaduni, ili kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikilizana kwa makini; kwa kuheshimiana na kuthaminiana, tayari kumwilisha tunu msingi za maisha ya Kiinjili zinazofumbatwa katika nadhiri, maisha ya kijumuiya, sala na udugu katika Kristo.

Watawa watambue kwamba, maisha yao ni kielelezo cha fumbo la Mungu mbele yao, ndiyo maana Maaskofu wanapenda kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Kristo na Kanisa, ili aweze kuwashirikisha upendo wake kwa Mwanaye mpendwa Yesu Kristo, tayari kujisadaka kila siku ya maisha yao, ili kushiriki katika mchakato wa kazi ya Ukombozi wa binadamu. Hivi ndivyo Baraza la Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika linavyohitimisha barua yake ya kichungaji kwa ajili ya maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.