2015-01-30 08:10:55

Kimbembe cha uchaguzi mkuu Nigeria!


Wananchi wenye hasira kali, Alhamisi, tarehe 29 Januari 2015 wameutupia mawe msafara wa Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria kwa Serikali yake kushindwa kudhibiti vitendo vya kigaidi vinavyofanywa na Boko Haram, wakati wao wakijihakikishia usalama. Zaidi ya watu 10, 000 wamekwisha poteza maisha, lakini viongozi wa Serikali wanaendelea kujikita katika kampeni ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika hapo tarehe 14 Februari 2015.

Wakati huo huo, Tume huru ya uchaguzi nchini Nigeria imekataa wazo la Rais Jonathan la kutaka kuhairisha uchaguzi mkuu kutokana na sababu za kiusalama, hasa katika maeneo ambayo kwa sasa yanashukiliwa na Kikundi cha kigaidi cha Boko Haram. Tume huru ya uchaguzi inasema, tayari imekwisha chunguza maeneo ya hatari na kwamba, uchaguzi utafanyika kama ilivyopangwa, kwa kuandaa maeneo ambayo yatakuwa salama ili kuhakikisha kwamba, wananchi wanatumia haki yao ya kikatiba kuchagua viongozi wanaowataka.

Hadi sasa kuna vyama 28 vya kisiasa nchini Nigeria vinavyowania uchaguzi mkuu nchini humo. Rais Jonathan anakabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa Jenerali Muhammadu Buhari. Tume huru ya uchaguzi itaendelea kushirikiana na wadau mbali mbali nchini humo ili kuhakikisha kwamba, uchaguzi unakuwa huru na wa haki.







All the contents on this site are copyrighted ©.