Katekesi na Uinjilishaji ni sawa na uji kwa mgonjwa!
Askofu mkuu Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la uhamasishaji wa Uinjilishaji
mpya anasema, Katekesi na Uinjilishaji mpya ni chanda na pete, kwani ni mambo makuu
mawili ambayo kamwe hayawezi kutenganishwa na kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anaendelea
kulihamasisha Kanisa kujikita katika uinjilishaji mpya kwa njia ya ushuhuda wa maisha
yanayomwilishwa katika imani tendaji! Hii ndiyo njia makini ya waamini kuweza kuwashirikisha
jirani, imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.
Katekesi ya kina haina budi kujikita
katika maisha ya kiroho, ili kwamba, mafundisho tanzu ya Kanisa yasaidia mchakato
wa toba na wongofu wa ndani; tayari kwa waamini kuweza kushuhudia mahusiano ya kukutana
na Yesu Kristo Mkombozi wa ulimwengu. Haya ni kati ya mambo ambayo yameibuliwa hivi
karibuni wakati wa kongamano la siku mbili lililokuwa limeandaliwa na Baraza la Kipapa
la uhamasishaji wa uinjilishaji mpya na wakuu wa Tume za Katekesi kutoka katika Shirikisho
la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya. Wajumbe wamewezesha kushirikishana uzoefu,
mang'amuzi na changamoto wanazokabiliana nazo katika mchakato wa ufundishaji wa katekesi
makini miongoni mwa Watu wa Mungu.
Baba Mtakatifu Francisko anawataka Makatekista
kuwa watangazaji na mashuhuda makini wa Habari Njema ya Wokovu na kwamba, Katekesi
ni chombo cha Uinjilishaji mpya na kwamba, Katekesi haina budi kuambatana na tasaufi
ya maisha ya kiroho; kama inavyofafanuliwa kikamilifu katika Waraka wa Baba Mtakatifu
Francisko, Injili ya Furaha, Evangelii gaudium. Katekesi haina budi pia kujikita katika
mawasiliano ya kina na Yesu Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Shirikisho la Mabaraza
ya Maaskofu Ulaya, lina zaidi ya Makatekista nusu millioni, wanaojisadaka kila siku
kwa ajili ya kuwafundisha na kuwarithisha watoto, imani, maadili na tunu msingi za
maisha ya Kikristo.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili
ya Radio Vatican.