Mkristo anapokutana na Yesu kwa mara ya kwanza katika maisha yake, hana budi kutunza
ndani mwake kumbu kumbu na matumaini, yanayomkirimia ujasiri wa kusongea mbele pasi
na woga wala makunyanzi, tayari kushuhudia imani yake hata katika mazingira magumu.
Siku hii ni mwanzo wa kukutana na mwanga wa Kristo katika maisha, tukio ambalo
linaujaza moyo wa mwamini furaha ya ajabu, kiasi hata cha kutamani kuthubutu kutenda
makuu. Mwamini hana budi kuendelea kukuza na kuimarisha ujasiri, ari na ukweli; mambo
yanayoibuliwa katika upendo wa kukutana na Yesu kwa mara ya kwanza katika maisha!
Hii
ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika Ibada ya Misa
Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, siku ya Ijumaa,
tarehe 30 Januari 2015, changamoto na mwaliko kwa waamini kusonga mbele kwa ujasiri
mkubwa, kwa kutambua kwamba, upendo wa Yesu unawaongoza.
Baba Mtakatifu anasema
kwamba, Wakristo wasiokuwa na msimamo ni hatari sana kwani ni sawa na "Mbwa anayekula
matapishi yake" na kundi la pili ni wale waamini ambao kwa mara ya kwanza wanaonesha
furaha kwa kuona miujiza inayotendwa na Yesu, lakini wanapokabiliwa na magumu pamoja
na changamoto za kiimani, wanasinyaa na kukosa mwelekeo; hawa ndio wale ambao baada
Shetani kubomolewa makazi yake katika maisha yao, anapowarudia tena, hali yao inakua
mbaya zaidi, kuliko ilivyokuwa hapo mwanzo, kama anavyosimulia Yesu mwenyewe katika
Maandiko Matakatifu. Waamini waoneshe ujasiri wa kushinda ubaya kwa kutambua kwamba,
matumaini kwa Yesu, kamwe hayawezi kumdanganya mwamini.
Kumbu kumbu hai na
matumaini anasema Baba Mtakatifu ni kanuni msingi katika kutunza wokovu ambao ni zawadi
kutoka kwa Yesu, kwa waja wake, kwani mambo haya ni chemchemi ya imani, ili kuiwezesha
mbegu ya haladali kuweza kuzaa matunda ajaa. Inasikitisha kuona kwamba, katika hija
ya maisha, kuna Wakristo wengi ambao wamejikatia tamaa na kuanguka, kiasi cha kushindwa
kuonana na Yesu tena, kwani wamepoteza ile kumbu kumbu hai na matumaini.
Baba
Mtakatifu anawaalika waamini kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwasaidia kutunza
zawadi ya wokovu waliyoipokea kwa njia ya imani.