Katika kipindi cha Mwaka 2013 zaidi ya vijana 20, 000 Barani Ulaya walinyanyaswa kijinsia
kwa njia ya mitandao ya kijamii ambayo kwa sasa ni maarufu sana katika maisha ya vijana
wengi, kiasi kwamba, kwa kijana ambaye hashiriki kikamilifu katika mitandao ya kijamii
anaonekana kuwa ni mtu aliyepitwa na wakati.
Hili ni tatizo
linalokuwa na kuongezeka siku kwa siku na madhara yake ni makubwa katika maisha, malezi
na makuzi ya vijana wanaoogelea katika mitandao ya kijamii!
Baraza la Kipapa
la haki na amani kwa kushirikiana na wadau mbali mbali, hivi karibuni limezindua mbinu
mkakati wa kupambana na nyanyaso za kijinsia kwenye mitandao, kama sehemu ya maadhimisho
ya Kumbu kumbu ya Miaka 25 tangu Umoja wa Mataifa ulipotoa Azimio ya Haki ya Mtoto
Duniani.
Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani
anasema kwamba, malezi na makuzi ni jambo ambalo linapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza
kwa vijana, ili kuzuia majanga makubwa katika maadili na utu wema yanayoweza kuibuliwa
kwa matumizi haramu ya mitandao ya kijamii.
Vijana wanapaswa kuelimishwa kutambua
utu na heshima inayojikita katika maisha ya vijana wenzao, kwa kuwaona kuwa ni wenzi
wa maisha badala ya mwelekeo wa sasa wa vijana kutaka kupimana nguvu na kutishiana
maisha kwa njia ya mitandao, mambo ambayo yanasababisha madonda makubwa katika maisha
ya baadhi ya vijana. Vijana wasaidiwe kukuza na kudumisha mshikamano wa umoja, udugu
na upendo, kwa kutambua kwamba, wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu.
Kampeni
hii, inasimamiwa na kuendeshwa na Shirikisho la Vyama vya Watoto Wakatoliki, ambalo
limekwishakusanya sahihi zaidi ya elfu kumi zinazounga mkono kampeni hii, kama anavyoeleza
Bwana Olivier Duval, Rais wa Shirikisho hili wakati wa uzinduzi wa kampeni hii. Anasema,
kuna haja kwa jamii kulivalia njuga tatizo hili kwani ni hatari sana kwa malezi na
makuzi ya vijana kwa sasa na kwa siku za usoni.
Ni tabia inayowapelekea vijana
kuvunja sheria na kanuni maadili. Kumbe, kuna haja ya jamii kuwapatia vijana hawa
njia mbadala zitakazowalinda ili wasitumbukie wala kuwatumbukiza vijana wenzao katika
nyanyaso za kijinsia kwa njia ya mitandao ya kijamii, mambo ambayo yamewaachia vijana
wengi machungu makubwa katika maisha na makuzi yao.
Mama Flaminia Giovanelli,
Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la haki na amani anasema, maendeleo ya sayansi
na teknolojia ya habari ni makubwa sana, kiasi ambacho kinawataka wazazi na walezi
kushikamana na vijana wao, ili kuwapatia malezi bora, kwa kuangalia utajiri unaopatikana
kutoka katika matumizi ya mitandao ya kijamii na madhara yake. Mitandao ya kijamii
inaweza kuwa ni mahali ambapo vijana, wazazi na walezi wanakutana, ili kukuza na kudumisha
mahusiano ya kifamilia.
Lakini ukweli wa mambo unaonesha kwamba, mitandao
ya kijamii imekuwa ni uwanja wa mapambano na patashika nguo kuchanika kati ya vijana
na wazazi wao; ni mahali ambapo ubinafsi na uchoyo vimeshika nafasi ya kwanza. Kumbe,
kuna haja ya kuwa na matumizi bora zaidi ya mitandao ya kijamii, ili kweli isaidie
kukuza na kudumisha tunu bora za maisha ya kijamii kwa kuzingatia kanuni maadili na
utu wema.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio
Vatican.