2015-01-29 12:04:58

Msiwabeze wengine!


Yesu ameanzisha njia mpya ambayo wafuasi wake wanapaswa kuifuata kwa kuzingatia kwanza kabisa kwamba, wanahamasishwa kuwashirikisha na kuwamegea jirani zao imani, matumaini na mapendo; ili kuepuka kishawishi cha baadhi ya watu kutaka kubinafsisha imani ambayo ni mlango wa wokovu. Wote wamekombolewa na Yesu, lakini Yesu anamfahamu kila mtu kwa jina, kwani amemwona, akamtambua na hatimaye, akayamimina maisha yake.

Mwenyezi Mungu tangu mwanzo amependa kumkomboa mwanadamu kwa njia ya taifa teule, kama alivyofanya kwa Ibrahim, Baba wa imani, changamoto kwa waamini kusaidiana na kutaabikiana, kwani kishawishi cha kutaka kubinafsisha wokovu ni njia iliyopotoka. Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, Alhamisi, tarehe 29 Januari 2015.

Baba Mtakatifu anasema, imani inayojikita kwa Yesu inawasafisha waja wake; matumaini yanawawezesha kupata ahadi za Mungu na hivyo kuendelea kusonga mbele pasi na kukata tamaa na kwamba, mapendo yanawawezesha waamini kusaidiana kwa njia ya matendo ya huruma. Kumbe, imani ni zawadi inayowasukuma waamini kuwashirikisha wengine na wala si jambo la mtu binafsi, bali inapania wokovu wa wote.

Baba Mtakatifu Francisko anaonya tabia ya baadhi ya waamini kudhani kwamba wao ni bora zaidi kuliko jirani zao. Jumuiya ya waamini inapoanza kumeguka katika makundi madogo madogo ni dalili za watu kutaka kubinafsisha wokovu ambao kimsingi ni zawadi ya wote. Ikumbukwe kwamba, Mwenyezi Mungu anapenda kuwaokoa watu na wala si tu kikundi cha wateule wachache.

Wakristo wana changamotishwa kuchunguza dhamiri zao, ili kuangalia kama wamekumbwa na jinamizi la ubinafsi katika maisha yao ya kiroho au wanajisadaka kwa ajili ya kuwamegea wengine imani, matumaini na mapendo? Waamini wanaalikwa na Baba Mtakatifu Francisko kujisikia daima kuwa ni Taifa la Mungu, ambalo kila mtu amekombolewa na Mwenyezi Mungu anamtambua kwa jina lake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.