2015-01-29 12:06:30

Mh. Padre Jean-Bertin Nadonye Ndongo ateuliwa kuwa Askofu wa Jimbo la Lolo, DRC


Baba Mtakatifu Francisko amekubali ombi la kung'atuka kutoka madarakani lililowasilishwa kwake na Askofu Ferdinand Maemba Liwoke wa Jimbo Katoliki Lolo lililoko DRC kadiri ya Sheria za Kanisa namba 401 Ibara ya 1. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu amemteua Mheshimiwa Padre Jean-Bertin Nadonye Ndongo wa Shirika la Ndugu Wadogo wa Mtakatifu Francisko, kuwa Askofu mpya wa Jimbo la Lolo. Hadi uteuzi huu, Askofu mteule, alikuwa anafanya utume wake kwenye Makao makuu ya Shirika mjini Roma.

Askofu mteule Jean-Bertin Nadonye Ndongo alizaliwa tarehe 24 Machi 1965 huko Botuzu, Jimbo Katoliki la Molegbe. Baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa na kikasisi nchini DRC, akaweka nadhiri za kwanza tarehe 17 Septemba 1989 na nadhiri za daima hapo tarehe 17 Septemba 1992 na hatimaye, kupadrishwa kunako tarehe 2 Agosti 1993.

Tangu wakati huo amebahatika kutekeleza utume wake wa Kikuhani kama: Paroko Msaidizi, Gombera Msaidizi, Mlezi wa Wanovisi; Mshauri mkuu wa mkuu wa Kanda ya DRC, Paroko, Mlezi na Gombera; Msaidizi na baadaye mkuu wa Kanda ya Wakapuchini DRC na Rais wa Baraza la Wakapuchini Afrika ya Kati na Afrika Magharibi.

Amewahi pia kuwa Rais wa Baraza la Utawala wa Taasisi ya Mtakatifu Agostin, Kinshasa. Na kuanzia mwaka 2011 hadi mwaka 2012 alikuwa ni Rais wa Shirikisho la Wakuu wa Mashirika, DRC. Kuanzia mwaka 2012 hadi kuteuliwa kwake alikuwa ni Mwamuzi mkuu wa Wakapuchini, kwenye Makao makuu ya Shirika mjini Roma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.