Baraza la Kipapa la uhamasishaji wa Uinjilishaji mpya kwa kutambua umuhimu wa katekesi
makini katika mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika: Imani, Sakramenti za
Kanisa, Maisha adili na Sala, hivi karibuni, limekuwa na mkutano pamoja na wajumbe
kutoka katika Tume za Katekesi za Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, ili kujadili,
kupembua na kuangalia jinsi ya kuwasaidia waamini wanaotafuta maana katika maisha
yao!
Wajumbe kwa pamoja wamekazia umuhimu wa kuwapatia majiundo makini wakatekumeni,
ili waweze kuifahamu na hatimaye, kuikumbatia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.
Kuna watu wengi ambao wanataka kuifahamu imani yao kwa kina na mapana, ili waweze
kusimama imara, kuiungama, kuiadhimisha, kuimwilisha na kuisali, lakini wanakumbana
na mazingira ambayo ni hatari katika ukuaji wa maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili.
Mawazo
mepesi mepesi, tabia ya kubeza dini na watu kumezwa mno na malimwengu ni kati ya mambo
ambayo kwa sasa yanaoneka kana kwamba, ndio mfumo wa maisha ya wananchi wa Ulaya,
hali ambayo inajionesha pia katika utepetevu wa imani miongoni mwa Wakristo Barani
Ulaya, anasema Askofu mkuu Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la uhamasishaji
wa Uinjilishaji Mpya.
Anasema, kuna haja kwa Mama Kanisa kuimarisha uelewa
wa Mafundisho Tanzu ya Kanisa; mikakati na shughuli za kichungaji zinazotekelezwa
na Kanisa mahalia sanjari na ukuaji wa Mkristo mmoja mmoja katika maisha ya kiroho,
kiutu na kimaadili mintarafu katekesi ya kina. Ikumbukwe kwamba, katekesi ni muhtasari
wa mafundisho ya Kanisa yanayojikita katika kanuni ya Imani, maisha ya Kisakramenti,
Amri kumi za Mungu na Sala za Kanisa; hii ndiyo mihimili mikuu inayodhihirisha na
kushuhudia imani na maisha ya Kanisa.
Mchakato wa Uinjilishaji mpya unapania
kukuza na kudumisha ari na moyo wa shughuli na mikakati ya kimissionari; mambo ambayo
Baba Mtakatifu Francisko anasema yanamwilishwa katika Katekesi, inayomwezesha mwamini
kutolea ushuhuda imani yake kwa Kristo na Kanisa lake, tayari kujikita katika toba
na wongofu wa ndani, ili kukumbatia maisha mapya.
Uinjilishaji mpya unalihamasisha
Kanisa kutoka kifua mbele, ili kuwashirikisha Watu wa Mataifa, utajiri unaofumbatwa
katika maisha na utume wake, ili kuwawezesha watu kukutana na Yesu Kristo Mkombozi
wa dunia, tayari kuonja huruma na upendo wake usiokuwa na kifani. Mkutano huu umewashirikisha
Maaskofu wakuu wa Idara na Tume za Katekesi kutoka katika Shirikisho la Mabaraza ya
Maaskofu Katoliki Ulaya, CCEE.
Taarifa za wajumbe zinaonesha jinsi ambavyo
Makanisa mahalia yanavyotoa kipaumbele cha pekee kwa ajili ya katekesi sanjari na
kuhakikisha kwamba, Makatekista wanafundwa vyema, ili waweze kutekeleza dhamana na
utume wao barabara.
Ikumbukwe kwamba, Makatekista ni kundi muhimu sana katika
maisha na utume wa Kanisa, hawa ndio wanaofundisha imani, wanaowaandaa watoto, vijana
na wakatekumeni kupokea Sakramenti za Kanisa. Ni watu wanaojisadaka kwa ajili ya kufundisha
dini shuleni na parokiani, wakiheshimiwa na kuthaminiwa, watachangia kwa kina na mapana
katika katekesi, maisha na utume wa Kanisa.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.