Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa FAO, linaiomba Jumuiya ya Kimataifa
kuchangia kwa hali na mali ili kuikwamua Malawi, ambayo kwa siku za hivi karibuni
imekumbwa na mafuriko makubwa ambayo yamesababisha maafa na uharibifu mkubwa wa miundo
mbinu, mambo ambayo yanahatarisha uhakika wa usalama wa chakula nchini Malawi.
Taarifa
zinaonesha kwamba, zaidi ya watu 170, 000 wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana
na mafuriko, bado kuna watu 153 kutoka Wilaya ya Nsanje, hawajulikani mahali walipo.
Inasemekana kwamba, zaidi ya watu 116, 000 wamepoteza mazao na mifugo yao. Sehemu
kubwa ya ardhi imemezwa na mafuriko, kiasi kwamba, Serikali imetangaza hali ya hatari
kwa Wilaya 15 kati ya 28. Wilaya za Chikwawa, Nsanje na Phalombe zimeathirika vibaya
sana.
Serikali ya Malawi inakadiria kwamba, kunahitajika walau kiasi cha dolla
za kimarekani millioni 16 ili kusaidia kuokoa sekta ya kilimo na mifugo nchini humo.
Kama Malawi haitapatiwa msaada haraka iwezekanavyo, kuna hatari kwamba, itakumbukwa
na baa la njaa kwa siku za usoni, kwa kutambua kwamba, asilimia 86% ya wananchi wa
Malawi wanategemea maisha yao kutoka katika sekta ya kilimo.