Kitendo cha Zakariya Ismail Hersi, aliyekuwa kiongozi mkuu wa inteligensia ya Kikundi
cha kigaidi cha Al-Shabaab, ambacho kwa miaka ya hivi karibuni kimeitikisa Somalia
na nchi jirani kutokana na mashambulizi ya kigaidi, kuamua kubwaga manyanga na kuacha
kujihusisha tena na matumizi ya nguvu na badala yake, kuwataka, wanajeshi wa Al-Shabaab,
kuanza mchakato wa upatanisho, ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa,
kimepokelewa kwa matumaini makubwa.
Wachunguzi wa mambo wanasema, kifo cha
Godane aliyekuwa ni kiongozi mkuu wa Al-Shabaab, mwezi Septemba, 2014 kimeacha pengo
kubwa, kwani kiongozi huyu alikuwa anatawala kwa mkono wa chuma, hali ambayo imepelekea
mgawanyiko ndani ya Kikundi cha Al-Shabaab.
Serikali ya Somalia kwa kusaidiwa
na Vikosi vya ulinzi na usalama kutoka Umoja wa Afrika inaendelea kutawala sehemu
kubwa ya Somalia, licha ya mashambulizi ya mara kwa mara yanayofanywa na kikundi cha
Al-Shabaab. Wapenda amani, sehemu mbali mbali za dunia wamezipokea habari hizi kwa
matumaini makubwa!