2015-01-28 08:22:34

Waamini iweni visiwa vya huruma na upendo wa Mungu!


Imarisheni mioyo yenu ndiyo kauli mbiu inayoongoza ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2015 unaokazia kwa namna ya pekee mshikamano wa udugu na upendo kati ya Familia ya Mungu; umuhimu wa kuhangaikiana na kutaabikiana kama watu wa familia moja, kwa kusaidiana katika raha na shida; kwa sala na kufunga.

Ni katika mwelekeo huu hapo tarehe 13 na 14 Machi 2015, waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee kumtolea Mungu muda wa masaa 24 na kwamba, inawezekana kufanya matendo ya huruma kila mtu kadiri ya uwezo wake. Lengo anasema Baba Mtakatifu ni kuhakikisha kwamba, mwamini anajitahidi kuunda moyo wake kadiri ya mapenzi ya Mungu. Kwaresima, kiwe ni kipindi cha huruma na upendo kwa kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu kwa kipindi cha Kwaresima, umezinduliwa na viongozi wakuu wa Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum, wakisaidiana na DR. Michel Roy, Katibu mkuu wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis. Kwaresima ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani, kinachomwezesha mwamini kujikita katika matendo ya huruma kwa kuguswa na mahangaiko na shida za jirani yake, ili kuondokana na kishawishi cha utandawazi usiokuwa na mvuto wala mashiko katika maisha ya watu.

Askofu mkuu Giampietro Dal Toso, Katibu mkuu wa Cor Unum anasema, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wa Kwaresima anakazia maeneo makuu matatu yanayoweza kumsaidia mwamini kuvuka tabia ya kutowajali wengine: kwanza kabisa ni ndani ya Kanisa, Jumuiya ya Waamini na katika maisha ya kila mwamini.

Hapa kunahitajika wongofu wa ndani, ili kuweza kumtambua Kristo aliyejisadaka kwa ajili ya umaskini wa binadamu, ili kuanza mchakato wa kufanana naye. Huu ni mwaliko wa kuachana na tabia ya ubinafsi na uchoyo inayomfanya mtu kujifunga katika undani wa maisha yake, kumbe imani iwe ni chombo kinachomsaidia mwamini kujitahidi kumfahamu Kristo, ili aweze kuwahudumia jirani zake wanaoteseka kutokana na shida mbali mbali za kiroho na kimwili.

Jumuiya za Kikristo zinachangamotishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, zinakuwa kweli ni visiwa vya huruma na upendo wa Mungu; mahali ambapo watu wanataabikiana, kusumbukiana na kuhudumiana kama ndugu. Waamini watambue kwamba, wao ni viungo hai vya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa, kumbe wanapaswa kuongoka, kubadilika, kukua na kukomaa, kwa kushirikishana neema na baraka kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.

Cor Unum itaendelea kuwa ni chombo cha upendo na huruma ya Baba Mtakatifu kwa watu wanaofikwa na majanga sehemu mbali mbali za dunia, lakini kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kama ilivyojitokeza huko Haiti kwa kuchangia kiasi cha dolla za kimarekani millioni 21.5 kwa ajili ya ujenzi wa Haiti iliyokumbwa na tetemeko la ardhi, miaka kadhaa iliyopita. Msaada na upendo wa Baba Mtakatifu umewafikia hata Familia ya Mungu huko Mashariki ya Kati na Ufilippini.

Monsinyo Segundo Tejado Munoz, Katibu mkuu msaidizi wa Cor Unum anasema, licha ya kiasi cha fedha kinachotolewa, lakini pia inapaswa kukumbuka kwamba, kuna umati mkubwa wa watu wanaojisadaka kwa ajili ya kuwahudumia wakimbizi, wahamiaji, wagonjwa na wazee, hawa thamani na mchango wao hauwezi kupimwa kwa njia ya fedha, imani inayomwilishwa katika matendo, ndiyo changamoto kubwa inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema.

DR. Michel Roy, Katibu mkuu wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis anasema kwamba, wao wataendelea kusikiliza na kujibu kilio cha damu kwa njia ya utandawazi wa mshikamano wa mapendo, ili kuvuka mipaka ya utandawazi usiojali wala kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya watu. Maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ndiyo Manabii wa nyakati hizi, wanaopaswa kusikilizwa kwa umakini mkubwa.

Maskini ni hazina na utajiri wa Kanisa, changamoto kwa watu kutomezwa na malimwengu pamija na uchu wa kupenda mno fedha na mali. Waamini na watu wenye mapenzi mema, wawe makini katika utunzaji bora wa mazingira kwani madhara ya mabadiliko ya tabia nchi yamekuwa ni chanzo kikuu cha majanga asilia yanayoendelea kuwatumbukiza watu katika lindi la umaskini wa hali na kipato.

Ikumbukwe kwamba, bado kuna biashara haramu ya binadamu, uhalifu dhidi ya utu na heshima ya binadamu; biashara haramu ya silaha inaendelea kuchangia vita, migogoro na kinzani za kisiasa na kijamii sehemu mbali mbali za dunia na kwamba, kuna baadhi ya makampuni yanavuna rasilimali na malighafi kutoka katika nchi zinazoendelea duniani, lakini yanachangia kidogo sana katika pato ghafi la taifa. Upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu ni fadhila inayofungua milango ya matumaini kwa wale waliokata tamaa ya maisha.







All the contents on this site are copyrighted ©.