2015-01-28 14:20:30

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya IV ya Kipindi cha Mwaka wa B wa Kanisa


Mpendwa msikilizaji wa Neno, tukiwa pamoja tokea Radio Vatican, tunatafakari Neno la Mungu Dominika ya 4 ya mwaka B wa Kanisa. Mama Kanisa atualika kusadiki kina kuwa Bwana tuliyemtarajia, yu pamoja nasi na hivi kumfuata ndio wito wetu, ndio mwaliko wa Kikristo. RealAudioMP3

Mwandishi wa kitabu cha Kumbukumbu la Torati ambamo tunapata somo la kwanza
anatualika kutambua kuwa Mungu haachi kutimiza ahadi yake ya kale kwamba atamtuma Nabii atakayetangaza hukumu zake kwa haki, atakayesema yale ya Bwana na kama atasema kinyume atakufa. Manabii wengi walitangaza ujumbe wa Mungu lakini hasa katika zama zetu Mungu anasema nasi kwa njia ya Masiha kama ambavyo Wayahudi walielewa ujumbe huo wa Neno la Mungu.

Masiha yaani mkombozi ametufundisha yote na kutujalia Ubatizo na sakramenti nyingine. Kwa njia hiyo kama wana wa Pentekoste tunaalikwa kutangaza yaliyo ya Mungu na kama ni kinyume basi tutapotea katika njia zetu.

Mtume Paulo anapowaandikia Wakorinto katika barua yake ya I sura ya saba, anaweka wazi miito mbalimbali katika Kanisa na anataka kila mmoja afahamu kwa uhuru kamili, wajibu wake mbele ya wito huo katika kutekeleza mapenzi ya Mungu. Wito wa ndoa ni wito mtakatifu ambao wamweka mtu katika wajibu wa familia yaani kuhudumu familia na yote yahusuyo maisha ya ndoa.

Kwa jinsi hiyo, Mtume Paulo anaona wajibu huo usipotendwa kwa unyenyekevu na hekima waweza kumfanya mwanafamilia azame huko na kusahau wito wake wa kushughulikia masuala ya uinjilishaji. Suala muhimu ni kuwa makini kutambua kuwa ndoa ni kwa ajili ya huduma ya familia, Kanisa na Mungu mpaji.

Anatafakari juu ya wito wa upadre na maisha ya kitawa akisema kwa wito huu mmoja aweza katika umakini wake kushughulikia zaidi maisha ya missioni yaani kupeleka habari njema kwa mataifa. Awaalika wenye wito huu kuona kuwa wanawajibika zaidi kufungua mioyo yao kwa Mungu kwa ajili ya wokovu wa watu na wao wenyewe. Wakumbuke useja unatoa zaidi nafasi ya uwajibikaji katika shamba la mizabibu na hivi madai kwao ni makubwa zaidi kuliko wengine.

Mpendwa unayenisikiliza yafaa kukumbuka jambo moja, ikiwa mmoja atakuwa na mashaka upi ni wito mzuri au wa juu! Toka ndoa twampata Padre na mtawa na hivi Kristu ameweka Sakramenti zote katika uwiano mkamilifu akitakatifuza maisha ya watu kadri ya wito wa kila mmoja, yaani kadri ya karama na vipaji alivyomjalia.

Mwinjili Marko anaweka mbele yetu yule Nabii tuliyehaidiwa katika somo la kwanza atakayetangaza kazi ya Bwana. Bwana yuko katika utume na anawaponya wagonjwa, si kwa nguvu ya mazingaombwe bali kwa nguvu ya mkono wa Mungu. Anatangaza vita kinyume na pepo ambapo kwa kawaida ni ile hali ya kutokuwa na roho wa kweli na hivi wenye pepo wanakuwa bado hawajakutana na Bwana.

Anataka wana wa Mungu wasibaki chini ya utawala wa shetani bali wawe huru katika yeye. Kwa jinsi hiyo mara wakutanapo na Bwana lazima pepo wakimbie kwa sababu yupo aliye Mungu mwenye nguvu, mwenye ufalme mabegani mwake. Bwana anatoa sauti kali “fumba kinywa chako umtoke” hii yamaanisha ugomvi uliopo katika ya pepo wachafu na maisha safi ya Kikristo.

Basi mpendwa mwana wa Mungu tekelezeni mausia ya Bwana wakati wote ili kukaa katika wito wako kwa furaha na matumaini ukikumbuka kuwajibika kadiri ya wito huo katika kutenda yaliyo ya Mungu. Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari hii imeletwa kwako na Pd. Richard Tiganya C.PP.S








All the contents on this site are copyrighted ©.