Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini, linalaani matukio ya uvunjifu wa amani
na utulivu yaliyojitokeza huko Soweto, Afrika ya Kusini, kwa maduka ya wageni kuvunjwa
na watu kuwapora mali. Katika matukio haya kuna baadhi ya watu ambao wamepoteza maisha
na wengine wengi kujeruhiwa. Jeshi la Polisi linawashikilia watu zaidi ya 120 kuhusiana
na matukio haya na kwamba, kuna idadi kubwa ya wafanyabiashara waliokutwa na silha
kinyume cha sheria.
Uvunjifu wa amani na utulivu ulijitokeza hivi karibuni
pale ambapo kijana mmoja alipigwa risasi na kuuwawa na mfanyabiashara mmoja huko Soweto
katika tukio la kujaribu kupora. Maaskofu wanawataka wananchi kuzingatia utawala wa
haki na sheria na kamwe wasijichukulie sheria mikononi mwao, kwani wanaweza kusababisha
madhara makubwa kwa watu na mali zao. Vitendo vya kuvunja majengo na miundo mbinu
vinachangia hata kuharibu maadili na utu wema; mambo yanayolichafua taifa.
Maaskofu
wanasikitika kusema kwamba, katika matukio haya kuna watu ambao wamepoteza maisha
yao; wanasali na kuwaombea wale wote waliofikwa na majanga haya na wanapenda kuonesha
mshikamano wao wa dhati na wafanyabiashara ambao wameshuhudia maduka na biashara zao
zikiharibiwa na watu waliokuwa na hasira. Matukio yote haya yanaendelea kusababisha
machungu katika maisha ya watu.
Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini,
linawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuwasaidia wale ambao wameathirika
kutokana na matukio ya uvunjifu wa amani na utulivu huko Afrika ya Kusini. Wananchi
watoe ushirikiano wa dhati, ili wahusika waweze kufikishwa kwenye mkondo wa sheria.
Wazazi na walezi watambue dhamana na wajibu wa kuwalea watoto wao kwa kuzingatia kanuni
maadili na utu wema.