Msitumie nguvu ya fedha kukumbatia utamaduni wa kifo!
Kardinali Seàn O'Malley, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Boston, Marekani, amepongeza
uamuzi wa Serikali ya Marekani kutokutoa fedha ya walipa kodi kwa ajili ya kugharimia
vitendo vya utoaji mimba na kwamba, hii ni hatua muhimu sana katika mchakato wa kulinda
watoto ambao bado hawajazaliwa, jambo linaoonesha utashi wa wananchi wengi wa Marekani.
Sheria ya kufuta ruzuku ya serikali kwa ajili ya kugharimia vitendo vya utoaji
mimba, ilipitishwa tarehe 22 Januari 2015, wakati wa maandamano makubwa kupinga sheria
ya utoaji mimba nchini Marekani. Serikali kwa sasa inakazia umuhimu wa ukweli na uwazi
katika matumizi ya fedha za umma. Kardinali O'Malley anasema, umefika wakati kwa Serikali
kuheshimu maamuzi na sheria zake ambazo zimekuwepo nchini humo kwa takribani miaka
thelathini na saba na kwamba, isitumie nguvu ya fedha kuhamasisha vitendo vya utoaji
mimba na wala isiwalazimishe walipa kodi kuchangia mauaji.
Serikali ina wajibu
wa kuwasaidia watu kupokea zawadi ya maisha badala ya kuwahamasisha kutoa mimba. Umefika
wakati kwa wananchi wa Marekani kuchagua sera za bima ya afya zinazoendana na kanuni
maadili na utu wema.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili
ya Radio Vatican.