Baraza la Maaskofu Katoliki Pwani ya Pembe, limehitimisha mkutano wake wa mwanzo wa
mwaka, kwa kuwataka waamini na wananchi wote, kujikita katika ujenzi wa msingi wa
haki, amani, upatanisho na umoja wa kitaifa baada yao nchi kwa miaka kadhaa kuogelea
katika dimbwi la machafuko na vita; mambo ambayo yamepelekea maafa makubwa kwa watu
na mali zao.
Wananchi wanataka
kujikita katika mchakato wa haki, amani, msamaha na upatanisho wa kitaifa, kama chachu
ya kuwaletea maendeleo endelevu. Hii ni changamoto ya kuondokana na mawazo ya kuweza
kupata mafanikio katika maisha kwa kukumbatia ushirikina, ambao pia umekuwa ni chanzo
cha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia pamoja na uvunjifu wa mustakabali wa taifa.
Wananchi watakakiwa kufanya mabadiliko makubwa katika maisha yao kwa kukataa kishawishi
cha ulevi wa kupindukia, rushwa, ufisadi pamoja na kukumbatia utamaduni wa kifo.
Baraza
la Maaskofu Katoliki Pwani ya Pembe, linawahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi
mema, kujifungwa kibwebwe ili kuganga magonjwa ya kiroho, kimwili na ukosefu wa maadili
na utu wema. Maaskofu wanataka wananchi kutekeleza wajibu wao kikamilifu na wote kwa
pamoja, washikamane ili kupambana kufa na kupona na majanga ambayo yanaendelea kukwamisha
mchakato wa maendeleo ya watu: kiroho, kimwili na kimaadili. Serikali inawajibika
kupambana pia na rushwa pamoja na ufisadi, kwa kuhakikisha kwamba, utawala wa sheria
unajengeka na kudumishwa miongoni mwa wananchi.
Baraza la Maaskofu Katoliki
Pwani ya Pembe, linawataka wananchi kujenga na kudumisha haki, amani na utulivu, hasa
wakati huu wanapojiandaa kwa ajili ya uchaguzi mkuu. Wananchi wajikite katika ukomavu
wa maisha ya kiroho na kimaadili, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa tunu msingi
zinazowaunganisha wananchi wote wa Pwani ya Pembe. Wananchi wanaonywa tabia ya kuuza
ardhi kuwa ni hatari kwa maendeleo yao ya siku za usoni.
Baraza la Maaskofu
Katoliki Pwani ya Pembe, mwishoni, linawataka vijana kujikita katika tunu msingi za
kimaadili na utu wema na kukataa katu katu kutumiwa na baadhi ya wanasiasa uchwara
kwa ajili ya mafao yao binafsi. Vijana wajenge moyo na tabi ya kufanya kazi halali
na kwamba, hakuna sababu ya kukata tamaa kwani Pwani ya Pembe ni nchi ya matumaini,
wakitaka wanaweza kupata maisha bora zaidi.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.