2015-01-27 14:46:47

Ni utata mtupu!


Taasisi ya ndoa na familia inaendelea kukabiliana na matatizo na changamoto mbali mbali ambazo wakati mwingine zinataka kuhalalishwa kisheria, kwa kile kinachodaiwa eti ni uhuru wa mtu kujiamria mambo yake binafsi, hata kama kanuni maadili na utu wema vinawekwa rehani! RealAudioMP3

Askofu mkuu Eamon Martin wa Jimbo kuu la Armagh, Ireland anasema, Serikali nchini humo inatarajiwa mwezi Mei, 2015 kupiga kura ya maoni kuhusu uwezekano wa kuwa na ndoa za watu wa jinsia moja.

Mada hii ni nyeti na Kanisa linapenda kushiriki kikamilifu katika mchakato wa majadiliano haya, ili kutoa mchango na maoni yake kuhusiana na tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kama sehemu ya dhamana yake ya kuendelea kutangaza Injili ya Familia kwa Watu wa Mataifa, licha ya watu kuendelea kukengeuka na kumezwa na malimwengu yanayokwenda kinyume cha utu na heshima ya binadamu. Serikali iwahakikishie watu wote uhuru wa kuzungumza, bila matusi, kwa kuzingatia nguvu ya hoja, utu na heshima ya binadamu, kwani hapa tafsiri ya maisha ya ndoa na familia iko hatarini.

Askofu mkuu Martin anasema, msimamo na mafundisho ya Kanisa ni ndoa kati ya Bwana na Bibi, wanaojisadaka kwa njia ya upendo, ili kupokea na kuendeleza Injili ya Uhai kadiri ya mpango wa Mungu; wakiwa na dhamana ya malezi kwa watoto wao ambao kweli ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Kanisa linakazia mafao ya binadamu na kamwe si suala la mtu kujisikia kutokana na vionjo vyake; Kanisa linakazia mapngo wa Mungu katika maisha ya mwanadamu, kwa kutambua tofauti kati ya Bwana na Bibi na umuhimu wa watu hawa kukamilishana. Wazazi wawe na dhamana na haki ya kutoa malezi bora kwa watoto wao na kwamba, mkamilishano wa upendo, kati ya Bwana na Bibi ndiyo zawadi na siri kubwa ambayo Mwenyezi Mungu ameificha katika taasisi ya ndoa na familia na wala si vinginevyo!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.