Wakristo wengi mjini Niamey, nchiniNiger, Jumapili iliyopita wameadhimisha Ibada ya
Misa Takatifu na Liturujia ya Neno pasi na nguo wala vyombo vya ibada, baada ya Makanisa
kadhaa kuchomwa moto hivi karibuni kutoka na kinzani za kidini. Viongozi wa Kanisa
wanaendelea kuwahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutokata tamaa,
bali waendelee kujikita katika majadiliano ya kidini, ili amani, upendo na mshikamano
viweze kutawala tena katika mioyo ya watu kwa kuondokana na chuki pamoja na kinzani
za kidini, ambazo kwa sasa hazina mvuto wala mashiko kwa ustawi na maendeleo ya watu!
Viongozi
wa Kanisa wanasema, uharibifu uliofanywa kwenye Parokia za Jimbo kuu la Niamey, nchini
Niger ni zaidi ya millioni mbili za Euro. Ili kuonesha umoja na mshikamano wa Kikanisa,
waamini wa Jimbo kuu la Niamey wameamua kuchangia sehemu ya mshahara wao, ili kusaidia
mchakato wa ujenzi wa Parokia na nyumba za Ibada zilizochomwa moto hivi karibuni kutokana
na msimamo mkali wa kidini. Sehemu ya pili ya mchakato huu ni kuendeleza majadiliano
ya kidini, ili kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa kidugu.
Viongozi
wakuu wa Kanisa wameamua kutembelea Parokia zote Jimboni humo, ili kuwaimarisha waamini
katika msingi wa haki, amani, msamaha na upatanisho. Wakleri na waamini wanaendelea
kusali kwa ajili ya amani na utulivu, huku wakimwomba, Bikira Maria awaombee, ili
kweli waendelee kuwa ni watu wenye matumaini, upendo, msamaha na upatanisho. Licha
ya magumu na changamoto wanazokabiliana nazo, waamini na watambue kwamba, bado wanahamasishwa
kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya
wengi.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.