Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha,
kilichoko mjini Vatican, Jumanne, tarehe 27 Januari 2015 amekumbusha kwamba, ukosefu
wa utii na kushindwa kutekeleza mapenzi ya Mungu, kulimpelekea mwanadamu kukosa Paradiso
na kwamba, utii wa Adamu ulimfungulia njia ya mbinguni. Yesu Kristo anawafundisha
wafuasi wake kujikita katika utii, kwa kutekeleza mapenzi yake hapa duniani, tayari
pia kushiriki katika utukufu wake mbinguni.
Yesu katika maisha na utume wake
alionesha utii mkubwa kwa Baba yake wa mbinguni, lakini bila kusahau kwamba, Bikira
Maria ni mama aliyeonesha utii wa hali ya juu kwa Malaika Gabrieli, alipokubali mpango
wa Mungu katika maisha yake. Na kwa kukubali kwake, Bikira Maria akaanzisha safari
ya mshikamano na binadamu.
Baba Mtakatifu anasema, anaendelea kusali ili Mwenyezi
Mungu aweze kumkirimia ujasiri wa kufanya mapenzi yake, lakini zaidi kuyafahamu mapenzi
haya katika maisha na katika maamuzi ambayo anapaswa kuyafanya kwa wakati huu; namna
ya kuratibu mambo mbali mbali. Kimsingi, sala kwa ajili ya kufanya mapenzi ya Mungu
ni sala inayotaka kufahamu mapenzi hayo ya Mungu na kuyamwilisha katika uhalisia wa
maisha. Ni dhamana nyeti anasema Baba Mtakatifu.
Si rahisi kuyafahamu mapenzi
ya Mungu, kumbe, waamini wanapaswa kumwomba Mwenyezi Mungu, awakirimia neema ya kutambua
mapenzi yake na kuyatekeleza kama alivyofanya Yesu alipouambia umati mkubwa wa watu
uliokuwa unamsikiliza, mama na ndugu zake ni wale wote wanaotekeleza mapenzi ya Mungu.