Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu
ambaye amehitimisha hija yake ya kichungaji nchini Vietnam anasema kwamba, Vietnam
imebarikiwa kuwa na umati mkubwa wa Mapadre na Watawa, wanaoendelea kujisadaka kwa
ajili ya huduma kwa Mungu na jirani katika medani mbali mbali za maisha.
Waamini
walei, ni watu wenye ibada na upendo mkubwa kwa Kanisa na Wakleri wanaowahudumia.
Ni kundi ambalo linaendelea kushikamana na Kanisa katika maisha na utume wake. Kuna
ushirikiano mkubwa kati ya Kanisa na Serikali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao
ya wengi na kwamba, utume unaotekelezwa na Balozi wa Vatican asiye mkazi nchini humo,
unaendelea kuimarisha mahusiano kati ya Vietnam na Vatican.
Vietnam ni nchi
ambayo inaendelea kucharuka katika medani mbali mbali za maisha, changamoto ya kuendeleza
na kukuza majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali nchini humo, sanjari
na kukoleza moyo na ari ya kimissionari bila kusahau umuhimu wa utamadunisho, ili
kweli Injili ya Kristo, iweze kuota mizizi katika maisha na tamaduni za wananchi wa
Vietnam. Idadi ya Wakristo inazidi kuongezeka mwaka hadi mwaka nchini Vietnam, hili
pia anasema Kardinali Filoni, ni jambo la kumshukuru Mungu.
Kanisa katika mapambazuko
ya Millenia ya tatu ya Ukristo linapenda kuwekeza zaidi na zaidi Barani Asia kama
alivyokwishawahi kusema Mtakatifu Yohane Paulo II. Hii ni dhamana inayotekelezwa kwa
kujikita katika majadiliano ya kidini na kiekumene; haki na amani. Waamini wa Vietnam
wanamwomba Baba Mtakatifu Francisko, siku moja kuwatembelea ili aweze kuwaimarisha
katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaojikita kwa namna ya pekee kabisa katika ushuhuda
wa maisha.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio
Vatican.