2015-01-27 08:55:52

Fursa za ajira kwanza!


Kardinali Angelo Bagnasco, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, siku ya Jumatatu tarehe 26 Januari 2015 anawataka wanasiasa kuhakikisha kwamba, wanatoa kipaumbele cha kwanza kwa upatikanaji wa fursa za ajira miongoni mwa vijana, kwani madhara yake ni makubwa kwa familia nyingi. Vijana wengi wamekata tamaa ya maisha na kwamba, athari za myumbo wa uchumi kimataifa bado zinawatendea wengi kiasi hata cha kushindwa kutekeleza dhamana na wajibu wa kifamilia.

Kardinali Bagnasco amegusia pia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, mambo yatakatojadiliwa kwa kina na mapana wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia, itakayofanyika mwezi Oktoba, hapa mjini Vatican. Anasema, kumekuwepo na mjadala mkubwa Barani Ulaya kuhusu familia, lakini, kile kinachozungumzwa ni tofauti kabisa na tunu msingi za maisha ya familia asilia, inayoundwa katika mshikamano wa upendo kati ya bwana na bibi na wala si vinginevyo.

Watu watambue kwamba, haki inakwenda sanjari na wajibu; mambo ambayo kamwe hayawezi kutenganishwa. Kumbe kuna haja ya kuhakikisha kwamba, sera na mikakati ya Serikali inasaidia kujenga na kudumisha misingi bora ya kifamilia. Uhuru wa kujieleza na kuabudu ni mambo msingi katika jamii na kwamba, ni jambo lisilokubalika kiimadili kwamba, kuna Wakristo wanaoendelea kudhulumiwa, kunyanyaswa na kuuwawa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Misimamo mikali ya kidini inayoendelea kujitokeza Barani Ulaya na kuwa na mvuto kwa vijana wengi kutaka kujiunga ni changamoto ya kiimadili ambayo haina budi kufanyiwa kazi na Jumuiya ya Ulaya, ili kuona ni wapi ambako wamekosea na panatakiwa kufanyiwa marekebisho. Kuna utupu ambao Bara la Ulaya limejiundia na hivyo kutema tunu msingi za maisha ya kimaadili na kiroho zinazojikita katika: wema, ukweli na uzuri, utu na heshima ya binadamu vikipewa kipaumbele cha kwanza. Leo hii vitu vinapewa msukumo wa pekee, lakini utu na heshima ya binadamu vinawekwa rehani, jambo ambalo ni hatari kubwa.

Kardinali Bagnasco anasema, ni kosa kabisa Ukristo kutambulishwa na Nchi za Magharibi, kwani Injili inamwilishwa katika tamaduni na kamwe haiwezi kumezwa na tamaduni za watu na mazingira. NI kweli kwamba, tunu msingi za Kiinjili zimekuwa ni chachu ya utamaduni wa Bara la Ulaya na kwamba, zimetoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, kumbe kuna haja ya kujenga na kudumisha upendo, umoja na udugu kati ya watu. Kutokana na mantiki hii, mauaji ya kidini ni jambo lisilokubalika kamwe!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.