Baraza la Maaskofu Katoliki Poland, linaadhimisha Mwaka wa Upendo, kwa kutoa kipaumbele
cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili wao pia waweze
kuonja upendo na neema inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.
Familia ya
Mungu nchini Poland inaadhimisha tukio hili, miaka arobaini baada ya utawala wa Kikumonusti
kufutilia mbali kitengo cha misaada cha Kanisa Katoliki, Caritas nchini humo, kilichoanzishwa
baadaye kunako mwaka 1990.
Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki, Caritas ni
kati ya vitendo ambavyo vinafanya utume wake kwa ufanisi mkubwa katika Majimbo na
Parokia mbali mbali nchini Poland, hasa kwa ajili ya kuwasaidia na kuwahudumia maskini
na watu wanaopatwa majanga katika maisha. Ni kitendo ambacho kimeliwezesha Kanisa
kukesha na wagonjwa, wazee, watoto yatima na watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi.
Caritas imezijengea uwezo familia mbali mbali nchini Poland, ili ziweze kutekeleza
dhamana na wajibu wake wa kulea na kutunza watoto kadiri ya mpango wa Mungu.
Baba
Mtakatifu Francisko, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Mwezi Desemba, 2014, aliwakumbuka
waamini nchini Poland kwa kuadhimisha Mwaka wa Upendo, kwa kuonesha mshikamano na
maskini pamoja na wote wanaosukumbizwa pembezoni mwa jamii. Caritas katika maadhimisho
ya Jubilee ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwake tena nchini Poland, imeendelea kuwasaidia
watoto wengi wanaoishi katika mazingira hatarishi na magumu.
Baraza la Maaskofu
Katoliki Poland linabainisha kwamba, kipaumbele cha kwanza katika maadhimisho ya Mwaka
wa Upendo ni familia, ili kuziwezesha familia kujenga na kuimarisha tunu msingi za
maisha, ili hatimaye, kuziwezesha familia nchini humo kuwa kweli ni kitalu na shule
ya kwanza ya upendo na mshikamano kati ya watu!