2015-01-27 07:15:09

Boko Haram inaua hata chembe cha majadiliano ya kidini!


Askofu mkuu Ignatius Kaigama, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria anasema, wakati huu Nigeria inapojiandaa kwa ajili ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Februari, 2015, Kikundi cha Boko Haram kinaendelea kuzidisha mashambulizi ya kushtukiza na hivyo kusababisha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia.

Kuna hatari kwamba, Boko Haram ikatawala eneo lote la Kaskazini Mashariki mwa Nigeria na kwamba, lengo lao ni kuhakikisha kuwa wanatala mji wa Maiduguri. Ikiwa kama lengo hili litafanikiwa, miji mingine iliyoko kando kando ya Maiduguri itaanguka kwa urahisi sana.

Askofu mkuu Kaigama katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, si rahisi kuweza kufanya majadiliano ya kidini na Kikundi cha Boko Haram kwani hawa ni magaidi wanaoendelea kusababisha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia na hivyo kupandikiza mbegu ya chuki na uhasama kati ya Wakristo na Waislam. Na kwa maneno mengine, Boko Haram inaendelea kuvuruga mchakato wa majadiliano ya kidini nchini Nigeria.

Ni matumaini ya Maaskofu wa Nigeria kwamba, Jumuiya ya Kimataifa itaguswa na mahangaiko pamoja na mateso ya wananchi wa Nigeria na hivyo wataweza kuwaunga mkono katika mchakato wa kupambana na Boko Haram. Hii inatokana na ukweli kwamba, Serikali ya Nigeria imeonesha udhaifu mkubwa dhidi ya Kikundi cha kigaidi cha Boko Haram.

Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria linasema kwamba, uchaguzi mkuuu na atakayeingia madarakani si kipaumbele chao kwa sasa, Kanisa linapenda kuona viongozi watakaochaguliwa na wananchi kwa mwaka huu, wanakuwa kweli ni watu wanaotafuta mafao ya wengi, haki, amani, utulivu na maendeleo ya wananchi wa Nigeria. Inasikitisha kuona kwamba, ukosefu wa haki, amani na utulivu ni matunda ya rushwa na ufisadi.

Kwa bahati mbaya, viongozi wengi wa kisiasa nchini Nigeria wanatafuta mafao yao binafsi, ndiyo maana haya hawajishughulishi kikamilifu kutafuta haki, amani na utulivu na badala yake wanaendelea kujikita katika kampeni, ili wapate ridhaa ya kuongoza Nigeria. Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria kwamba, uchaguzi mkuu wa mwaka huu, utaweza kuwaamsha wananchi wa Nigeria kuchagua hatima ya maisha yao kwa siku za usoni, kwa kufanya maamuzi machungu, ili kuwapatia ridhaa viongozi watakaowaletea maendeleo ya kweli!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.