Imani ni zawadi kutoka kwa Roho Mtakatifu ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikirithishwa
kutoka kizazi kimoja hadi kingine, dhamana inayotekelezwa kwa uchaji mkubwa na wanawake.
Hayo yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri yake kwenye Kikanisa
cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican siku ya Jumatatu, 26 Januari 2015 wakati
Mama Kanisa alipokuwa anaadhimisha kumbu kumbu ya Watakatifu Timotheo na Tito.
Baba
Mtakatifu anasema, kuna tofauti kubwa ya kufundisha masuala ya imani, lakini imani
kimsingi ni zawadi ya Roho Mtakatifu ambayo imekuwa ikifanyiwa kazi na wanawake wachamungu
ndani ya familia, kwa kutambua kwamba, Bikira Maria amewazawadia walimwengu Mtoto
Yesu, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na kukaa kwake Bikira Maria.
Hivi ndivyo
alivyopenda Yesu, ili aweze kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.
Kumbe, imani inarithishwa kwa njia ya wanawake na kwamba waamini wanachangamotishwa
kuhakikisha kwamba, wanailinda na kuendelea kuiimarisha kwa njia ya Roho Mtakatifu,
vinginevyo imani inaweza kugeuzwa kuwa ni sehemu ya utamaduni.
Baba Mtakatifu
anawaalika waamini kuhakikisha kwamba, wanaachana na tabia ya woga na kamwe wasiionee
imani aibu, bali kusimama kidete ili kuweza kuishuhudia na kuiimarisha kwa njia ya
paji la nguvu, upendo na hekima, kwa kuwa na kiasi. Baba Mtakatifu anawaalika waamini
na watu wote wenye mapenzi mema kumwomba Mwenyezi Mungu ili awasaidie kuwa na imani
thabiti.