2015-01-26 08:48:43

Mchango wa ajili ya kusaidia Kanisa la Amerika ya Kusini


Wajibu wa kushirikishana imani ndiyo kauli mbiu ambayo imeiongoza Familia ya Mungu nchini Marekani kuanzia tarehe 24 hadi tarehe 25 Januari 2015 kukusanya mchango kama kielelezo cha umoja, upendo na mshikamano wa dhati na Kanisa la Amerika ya Kusini. Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani linakiri kwamba, waamini wa Kanisa la Amerika ya Kusini wanao mchango mkubwa sana katika ustawi na maendeleo ya Kanisa nchini Marekani.

Wao ni waamini ambao wamesheheni imani, wanayojitahidi kuwashirikisha na kuwamegea jirani zao. Maaskofu wanasema kwamba, licha ya Kanisa la Katoliki nchini Marekani kuchangia kwa hali na mali katika mchakato wa ustawi na maendeleo ya Kanisa la Amerika ya Kusini, lakini hata wao wanayo mengi ya kujifunza kutoka Amerika ya Kusini.

Mchango uliokusanywa na waamini kwa mwaka huu, utasaidia ujenzi wa Seminari za Majimbo nchini Colombia. Waamini wanaishukuru kwa namna ya pekee kabisa Familia ya Mungu nchini Marekani kwa kutokana na mchango wao wa hali na mali. Nyumba za malezi, zitasaidia kwa kiasi kikubwa katika majiundo na makuzi makini ya majandokasisi, tayari kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake kwa siku za usoni.

Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, limekwishachangia kwa kiasi kikubwa kwa ajili ya ujenzi mpya wa Kanisa nchini Haiti, wakati wa maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka mitano, tangu Haiti ilipokumbwa na tetemeko la ardhi na hivyo kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Kunako mwaka 2010, Baraza la Maaskofu lilichangisha kiasi cha dolla za kimarekani million 85 zilizosaidia kugharimia mahitaji muhimu kwa ajili ya wananchi wa Haiti.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.