2015-01-24 07:23:01

Ukardinali ni huduma!


Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia barua Makardinali wateule ishirini, watakaosimikwa rasmi hapo tarehe 14 Februari 2015, kwa kuwakumbusha kwamba, ukardinali ni wito katika huduma kwa Familia ya Mungu na wala si kilele cha taaluma wala kielelezo cha madaraka na ukuu. Baba Mtakatifu anawaalika Makardinali wateule, kuendelea kuonesha unyenyekevu unaojikita katika huduma makini kwa Familia ya Mungu.

Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu anawaalika Makardinali wateule kusherehea dhamana hii kwa kuwa na kiasi na kamwe wasimezwe na malimwengu na hivyo kuwaondoa kutoka katika mwelekeo sahihi wa Fumbo la Msalaba wa Kristo. Kwa kuteuliwa kuwa Kardinali kunamaanisha kwamba, wao sasa ni sehemu ya Jimbo kuu la Roma, ambamo wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuwa Mashuhuda amini wa Ufufuko wa Kristo, tayari kujisadaka wao wenyewe hadi tone la mwisho la damu yao, kama ikibidi.

Baba Mtakatifu anawaalika Makardinali wateule kujiandaa kupokea dhamana hii kwa sala na kufunga. Anawatakia amani na furaha na mwishoni, anawaalika kuendelea kumsindikiza katika maisha na utume wake kwa njia ya sala.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.