Wakimbizi na wahamiaji wanaoishi na kuhudumiwa kwenye kambi za wakimbizi nchini Kenya
wanahamasishwa kuhakikisha kwamba, wanaishi kwa amani na utulivu na kuachana tabia
ya chokochoko na uvunjaji wa sheria; mambo ambayo yamepelekea watu kadhaa kupoteza
maisha kwa siku za hivi karibuni.
Hii ni changamoto ambayo imetolewa hivi
karibuni wakati wa maadhimisho ya Siku ya wakimbizi na wahamiaji duniani na Askofu
Virgilio Pante, Mwenyekiti wa Tume ya Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya kwa ajili
ya wahamiaji, wakimbizi na mabaharia. Anasema, kunakosekana mchakato wa upatanisho
katika kambi za wakimbizi na wahamiaji, sanjari na kuendeleza misingi ya haki na amani.
Baba
Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa siku ya wakimbizi na wahamiaji anawataka
waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani,
udugu na mshikamano, sanjari na kukomesha mambo yanayosababisha vita, chuki na kinzani.