Walei wana mchango mkubwa katika ujenzi wa familia!
Baraza la Kipapa la Familia kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Sinodi ya Maaskofu
kuanzia tarehe 22 Januari hadi tarehe 24 Januari 2015 wameandaa kongamano la kimataifa,
linalovishirikisha vyama 80 ya kitume kutoka sehemu mbali mbali mbali za dunia, ili
kutoa mchango wao katika mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya
Familia, itakayofanyika mwezi Oktoba, 2015 hapa mjini Vatican.
Askofu mkuu
Vincenzo Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa la familia anasema kwamba, vyama vya kitume
vinamchango mkubwa katika kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.
Tema ya familia ni nyeti na muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa ndiyo maana,
matukio ya kifamilia yanafuatiliwa kwa udi na uvumba na vyombo vya upashanaji habari.
Ulimwengu
mamboleo umegubikwa sana na ubinafsi na uchoyo; mambo yanayochangia mipasuko na kinzani
za kijamii; ubaguzi na utenganio Kanisa halina budi kuwasaidia waamini kuwa kweli
ni mashuhuda wa Injili ya Familia, kwa maneno na matendo yao mema; yenye mvuto na
mashiko kwa jirani zao. Utamaduni mamboleo kwa bahati mbaya, umeendelea kubeza tunu
msingi za maisha ya ndoa na familia, kiasi cha kukosa mvuto kutoka kwa vijana wa kizazi
kipya, wanaopenda kuendelea kubaki nyumbani kwa wazazi wao na mbaya zaidi pasi na
kufunga ndoa, huku wakiendeleza uchumba sugu!
Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili
wa Vatican anasema, Askofu mkuu Vincenzo Paglia, wamewachangamotisha sana waamini
walei, kusimama kidete, kulinda, kutetea, kudumisha na kutangaza Injili ya Familia.
Familia inawajibu wa kusimama na kujitetea yenyewe dhidi ya mashambulizi kutokana
na utamaduni wa kifo na sera zinazosigana na mpango wa Mungu. Maadhimisho ya Sinodi
ya Maaskofu yanapania kuwajengea waamini uwezo wa kutangaza Injili ya Familia kati
ya Watu wa Mataifa.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili
ya Radio Vatican.