Uponywaji wa kimwili na Yesu ni ishara ya uponyaji mwingine muhimu zaidi... Papa
Alhamisi Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa Ibada ya Misa katika Kanisa dogo la
Mtakatifu Marta, homilia yake ililenga zaidi juu ya Injili ya siku (Marko 3: 7-12),
ambayo inaelezea jinsi makundi ya watu walivyokusanyika kutoka pande zote kwa lengo
la kuja kukutana na Yesu. Papa anasema watu wa Mungu waliona katika Bwana, kuna
"tumaini". Tumaini waliloliona katika njia zake za utendaji na mafundisho yenye kugusa
moyo , kwa sababu yalikuwa na nguvu ya Neno la Mungu.
Papa aliendelea kueleza
kwamba , watu walikuwa wamechoka na njia za ufundishaji wa walimu wa Sheria wa wakati
huo, ambao walibebesha zaidi mzigo mzito mabega mwa watu kwa amri nyingi, maagizo
mengi, ufundishaji amba o haukugusa mioyo ya watu. Lakini ufundishaji uliofanywa na
Yesu uligusa mioyo ya watu , kama ilivyokuwa hotuba yake mlimani juu ya Heri. Na
hivyo watu walichochewa na Roho Mtakatifu kwenda kumwona Yesu.
Papa
ameasa hata kwa nyakati hizi , Yesu bado yupo kati yetu. Lakini tunahitaji kuwa
na nia safi katika kumtafuta Yesu , si kwenda kumtafuta kwa nia ya uponyaji wa
maradhi ya kimwili tu, lakini nia hiyo ya kwenda kumtafuta ni lazima iwe safi tangu
mwanzo wake , kumtafuta kwa bidii kwa ajili ya uponywaji wa kiroho. Bahati mbaya
sisi binadamu hatufanyi bidii hiyo ya kumtafuta kwa manufaa ya kiroho , wala hatuna
muda na Mungu. Lakini katika hija ya kujitakasa, inatuhitaji kutenga muda wa kuwa
na Mungu. Papa alieleza akitazamisha kwa jinsi watu wengi huenda kumtafuta Mungu
katika madhabahu mbalimbali , lakini wengi wao, ni kwa ajili ya uponyaji wa mambo
ya kimwili , hujitupa miguuni mwake na kumgusa , ili uwezo wake uwaponye, lakini si
uponywaji wa Roho. .
Papa anasema, ziara za hija tunazofanya na isiwe kwa
sababu Yesu kuponywa mwili au matatizo. Unapaswa kutambua kuwa uponywaji wa mwili
ni ishara ya uponyaji mwingine, muhimu zaidi kuponywa kiroho, kama ilivyoandikwa
katika waraka kwa Waebrania (7:25), "Yesu ni daima ana uwezo wa kuwaokoa wale wanao
mkaribia Mungu katika njia yake, maana yeye anaishi milele akiwaombea kwa Mungu.
Papa
aliendelea kusema, ni muhimu leo hii, kutambua kwamba, Yesu amesimama mbele ya
Baba, akitolea sadaka maisha yake, kwa ajili ya wokovu wetu, anaonyesha majeraha
yake kwa Baba kama malipo ya wokovu wetu. Hivyo ndivyo ilivyo kila siku, Yesu anaingilia
kati katika maisha yetu , hutuombea. Nasi tunapaswa kila siku, na hasa wakati tunapoanguka
katika majaribu, kwa jambo moja au jingine, tukumbuke kwamba, yupo anayetuombea msamaha
kwa Mungu, anatuombea daima.
Papa ameonya kwamba kwa mara nyingi binadamu
husahau kwamba Yesu alikwenda Mbinguni, na kumtuma Roho Mtakatifu. Hii si simulizi
kama hadithi lakini ni ukweli halisi. Hata sasa, katika kila wakati, Yesu hutuombea.
Kila tunaposali sala hii: 'Bwana Yesu, nihurumie mimi mdhambi, Yeye hulichukua
ombi hili kwa Baba kwa ajili yetu.
Papa alieleza na kuhitimisha kwa kuomba
ili maisha yetu ya Kikristo, yaweze kuwa na imani zaidi kwamba tumeokolewa naye Yesu
Kristo ambaye kwa wakati huu ameketi upande wa kulia wa Baba, akituombea. Na akaomba
kwa Bwana , Roho Mtakatifu atuwezeshe kuelewa mambo haya.