2015-01-23 10:27:50

Uchomaji wa Makanisa ni kufuru!


Baraza la Makanisa Ulimwenguni limelaani na kusikitishwa na uharibifu mkubwa uliofanywa na baadhi ya waamini wenye misimamo mikali ya kiimani nchini Niger baada ya Jarida moja nchini Ufaransa kuchapisha picha za kashfa kwa dini ya Kiislam. Baraza la Makanisa Ulimwenguni linaipongeza Serikali ya Niger kwa kulaani vikali uvunjifu wa amani na uhuru wa kuabudu kwa visingizio vya misimamo mikali ya kidini.

Serikali ya Niger inawauliza waamini wa dini ya Kiislam, Je, Wakristo wamefanya nini hadi wastahili kupewa adhabu kubwa kiasi hiki. Je, ni ubaya gani ambao wametenda kiasi cha baadhi ya wananchi kuchoma Makanisa zaidi ya 70 pamoja na kusababisha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia? Niger ambayo kimsingi inakaliwa na waamini wengi wa dini ya Kiislam imekuwa ikiheshimu uhuru wa kuabudu, lakini katika miaka ya hivi karibuni, hali imeanza kubadilika na kwamba, kwa sasa kuna chuki za udini ambazo zinatokana na misimamo mikali ya kidini.

Viongozi mbali mbali wa Kikristo nchini Niger, wanawataka Wakristo kutolipiza kisasi kwani kutachochea vurugu, chuki na uhasama kati ya watu na badala yake, wajenge utamaduni wa kusamehe na kusahau; kupenda na kudumisha majadiliano ya kidini, kwa kutambua kwamba, wote ni ndugu wamoja, na tofauti zao za kidini na kiimani zisiwe ni chanjo cha vita, vurugu na kinzani. Waamini wawe ni mashuhuda wa imani kwa njia ya kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa, watu wachache wenye misimamo mikali ya kidini, kamwe wasipewe nafasi ya kuvura amani, utulivu na maridhiano kati ya watu kutokana na chuki na uhasama wa kidini.







All the contents on this site are copyrighted ©.