Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania amewapongeza wadau mbali mbali kutoka Barani
Afrika waliosaidia kukamilisha mchakato wa kuwaunganisha tena viongozi wakuu wa Chama
cha Ukombozi cha SPLM cha Sudan ya Kusini, kilichokuwa kimemeguka kutokana na machafuko
ya kisiasa kati ya Rais Salva Mayardit Kiir wa Sudan na Makamu wake Bwana Riek Machar;
tukio ambalo limetiwa sahihi mjini Arusha, tarehe 21 Januari 2015 na kuhudhuriwa na
umati mkubwa wa viongozi kutoka sehemu mbali mbali za Bara la Afrika.
Rais
Kikwete anasema, hii ni siku inayofungua ukurasa mpya wa matumaini ya amani na upatanisho
wa kitaifa na hivyo kusahau machafuko ya kisiasa yaliyoitumbukiza Sudan ya Kusini
katika vita ya wenyewe kwa wenyewe, kiasi cha kusababisha maafa makubwa kwa watu na
mali zao. Ukweli, uwazi, uvumilivu, mafao ya wengi na umoja wa kitaifa, ni mambo msingi
ambayo yamewezesha tena juhudi za majadiliano ya kina kuzaa matunda yanayokusudiwa.
Hiki sasa ni kipindi upatanisho, uponyaji na ujenzi wa Chama cha Ukombozi cha SPLM,
ili amani iweze kutawala tena na watu kujikita katika mchakato wa kujiletea maendeleo
yao wenyewe, changamoto kubwa kwa sasa ni kuhakikisha kwamba, mkataba huu unaimarishwa
na kudumishwa.
Rais Kikwete amewakumbusha viongozi hawa kwamba, kwa mara ya
kwanza haitakuwa vigumu, lakini waendelee kujenga utamaduni wa majadiliano na kutafuta
suluhu ya matatizo na changamoto watakazokutana nazo kwa amani na utulivu na kwamba,
kuna nchi za Kiafrika ambazo ziko tayari kusaidia mchakato wa amani, upatanisho na
maendeleo Sudan ya Kusini.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya
Kiswahili ya Radio Vatican.