Chuo kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki na Kati, CUEA kwa kushirikiana na Shirikisho
la Kimataifa la Vyuo vikuu vya Kikatoliki, IFCU, limechapisha kitabu kinachobainisha
njia mbadala ya kupambana na baa la umaskini, matunda ya utafiti uliofanywa kwa kipindi
cha miaka miwili, yaani kuanzia mwaka 2011 hadi mwaka 2012.
Utafiti huu umepembua
kwa kina na mapana mikakati, sera na programu za kupambana na baa la umaskini mintarafu
Serikali; mikopo nafuu inayotolewa kwa wajasiriamali pamoja na mikakati ya shughuli
za kichungaji zinazotekelezwa na Mama Kanisa kwa kujikita katika mshikamano na maendeleo
ya watu kwa kusaidiana katika umoja na upendo.
Utafiti huu unabainisha kwamba,
ili kweli umaskini uweze kupewa kisogo kwa wananchi wengi Barani Afrika kuna haja
ya kuhakikisha kwamba, kuna kuwepo: sera na mipango thabiti inayoratibiwa na kutekelezwa
na wadau mbali mbali na kwamba, mikakati ya kichungaji inayotolewa na Mama Kanisa
inaweza pia kuwa ni njia mbadala ya kupambana na baa la umaskini, linaloendelea kusababisha
majanga mengi Barani Afrika.
Huu ni mchango uliotolewa na Askofu mkuu Zacchaeus
Okoth, Mwenyekiti wa Tume ya haki na amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, wakati
wa kuzindua kitabu hiki. Askofu mkuu Okoth ameishauri Serikali ya Kenya kuangalia
tena sera, mikakati na programu ya marekebisho ya uchumi sanjari na mapambano dhidi
ya baa la umaskini nchini humo. Huduma zinazotolewa kwa njia ya mshikamano zimesaidia
hata watoto wa maskini kuendelea na masomo pamoja na kupata huduma msingi, kiasi cha
kusaidia katika mchakato wa maboresho ya maisha ya watu wengi hasa vijijini.
Ili
kupambana na umaskini wa hali na kipato, watafiti kutoka CUEA wanasema, kuna haja
kwanza kabisa kuhakikisha kwamba, mambo yote yanayosababisha na kupelekea kukua na
kuongezeka kwa umaskini wa hali na kipato yanashughulikiwa kikamilifu na kwamba, mshikamano
wa upendo unaoongozwa na kanuni ya auni katika utekelezaji wa mikakati ya shughuli
za kichungaji inayofanywa na Mama Kanisa ni njia muafaka ya kupambana na baa la umaskini
duniani.
Hapa kuna haja ya kushirikishana tunu msingi za maisha ya kiroho,
kiutu na kimaadili na kwamba, haitoshi kushirikishana rasilimali vitu na fedha tu!
Ukweli, uwazi na maendeleo na mafao ya wengi ni mambo msingi yanayopaswa kupewa kipaumbele
cha kwanza katika mapambano dhidi ya baa la umaskini. Wananchi wajenge utamaduni wa
kushirikishana baraka na tunu msingi za maisha!
Na Padre Richard A. Mjigwa,
C.PP.S Kwa msaada wa CISA, Nairobi, Kenya.