2015-01-22 12:32:40

Miaka 400 ya Uinjilishaji si haba!


Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu katika hija yake ya kichungaji nchini Vietnam, kuanzia tarehe 19 hadi tarehe 26 Januari, 2015 ameishukuru na kuipongeza Familia ya Mungu nchini humo kwa kushuhudia imani inayomwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa mahalia.

Wakatoliki nchini humo wanaendelea kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, katika medani mbali mbali za maisha, jambo ambalo linapaswa kupongezwa na kuendelea kuhamasishwa kwa waamini hasa wakati huu Mama Kanisa anapojielekeza katika mchakato wa Uinjilishaji mpya!

Waamini wamekuwa wakijikita katika maisha ya sala, tafakari ya Neno la Mungu, majiundo makini ya Katekisimu mpya ya Kanisa Katoliki na Mafundisho Jamii ya Kanisa, tayari kuyafanyia kazi katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu, kwa njia ya chachu na mwanga wa Injili ya Kristo. Waamini wanaonesha juhudi katika ujenzi wa Kanisa na Jamii katika ujumla wake.

Huu ni mwaliko anasema Kardinali Filoni kwa viongozi wa Kanisa nchini Vietnam kuhakikisha kwamba, wanawasaidia waamini kufahamu: dira, vipaumbele na mwelekeo wa Kanisa mintarafu Waraka wa Kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko, Injili ya Furaha. Familia ya Mungu nchini Vietnam inakumbushwa kwamba, chemchemi ya Uinjilishaji mpya inabubujika kutoka katika Furaha ya Injili, kwa kukutana na Yesu katika: Maandiko Matakatifu, Sakramenti za Kanisa; maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Waamini kwa kukutana na Yesu, wanachangamotishwa kuyapyaisha maisha yao ili kujikita zaidi katika dhamana na utume wa kimissionari, tayari kutoka kifua mbele ili kuwatangazia Watu wa Mataifa Injili ya Furaha na Matumaini.

Itakumbukwa kwamba, Uinjilishaji wa awali ni utume uliofanywa na Mashirika mbali mbali ya Kimissionari, waliopandikiza mbegu ya imani, matumaini na mapendo, leo mbegu hii imezaa matunda na kujimwilisha katika maisha ya waamini wa Vietnam. Kunako mwaka 2010 Kanisa Katoliki nchini Vietnam, limeadhimisha Jubilee ya Miaka 350 tangu Jimbo la kwanza lilipoanzishwa nchini humo na miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Vietnam. Mwaka 2015, Kanisa linafanya kumbu kumbu ya Jubilee ya miaka 400 ya Uinjilishaji! Hapa si haba!

Kardinali Filoni, anawakumbusha Maaskofu kwamba, dhamana yao ya kwanza katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza Watu wa Mungu ni Uinjilishaji unaoratibiwa kwa kina na mapana na Askofu mahalia, kwa kuwashirikisha na kuwahimiza waamini wote, kila mtu kadiri ya nafasi na wajibu wake kushiriki kikamilifu katika mchakato huu, huku wakiendelea kusali kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa zima.

Kardinali Filoni wakati anazungumza na Maaskofu Katoliki nchini Vietnam amewataka kuendelea kujikita katika mchakato wa Uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika majadiliano ya kidini na kiekumene, kwa kukazia ukweli, uwazi, ujasiri, uvumilivu na hekima kubwa. Mtumishi wa Mungu Francisko Xsaver Nguyen Van Thuan ni shuhuda wa matumaini na mtumishi mwaminifu wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Ni mfano hai wa kuigwa katika kutangaza Injili ya Kristo kwa njia ya ushuhuda wa maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.