Baba Mtakatifu Francisko anawatia ari na moyo mkuu waandaaji wa maandamano ya kutetea
Injili ya Uhai yanayotarajiwa kufanyika mjini Paris, Ufaransa, Jumapili ijayo tarehe
25 Januari 2015. Askofu mkuu Luigi Ventura, Balozi wa Vatican nchini Ufaransa anasema
kwamba, Baba Mtakatifu anawahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusimama
kidete kulinda na kutetea Injili ya Uhai kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao.
Wakati
huo huo, Baraza la Kipapa kwa ajili ya familia linabainisha kwamba, maisha ya binadamu
ni matakatifu, kumbe yanapaswa kuthaminiwa, kulindwa na kuendelezwa. Kutokana na changamoto
zinazoendelea kujitokeza dhidi ya tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, Baba Mtakatifu
Francisko anawahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kushiriki kikamilifu
pasi na kuchoka wala kukata tamaa katika mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa upendo
na Injili ya Uhai.
Maandamano haya ambayo yatafanyika siku ya Jumapili mchana
ni kielelezo cha Familia ya Mungu nchini Ufaransa kupinga utamaduni wa kifo unaofumbatwa
katika sheria za utoaji mimba; ili kuheshimu na kutangaza Injili ya uhai inayojikita
katika utamaduni wa upendo!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S Idhaa ya
Kiswahili ya Radio Vatican.