2015-01-21 09:03:41

Uchaguzi uwe wa: haki, kweli na huru!


Baraza la Maaskofu Katoliki Burkina Faso linaitaka Serikali nchini humo kuhakikisha kwamba, mchakato wa uchaguzi mkuu nchini humo unakuwa wa haki, kweli na huru na kwamba, Kanisa litaendelea kutekeleza dhamana na wajibu wake katika jamii pamoja na kujikita katika sala na ushauri, ili kweli: utu, heshima na mafao ya wengi yawe ni kati ya mambo yatakatopewa kipaumbele cha kwanza wakati wa uchaguzi mkuu, unaotarajiwa kufanyika nchini Burkina Faso, mwishoni mwa mwaka 2015.

Baraza la Maaskofu Katoliki Burkina Faso linabainisha kwamba, watu wanahitaji amani ambayo itakoleza mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu: kiroho na kimwili, baada ya Rais Blaise Compaorè kutawala nchi hii kwa kipindi cha miaka thelathini pasi na mabadiliko ya kina. Wananchi wa Burkina Faso wanatarajiwa pia kupiga kura ya maoni ili kupata Katiba Mpya, itakayokuwa ni: Sheria Mama, Mwongozo na Dira kwa nchi.

Maaskofu Katoliki katika mazungumzo na Bwana Michel Kafando, Rais wa Serikali ya mpito Burkina Faso, wameonesha wasi wasi si tu wakati wa kupiga kura bali hata baada ya kupiga kura kwani mara nyingi wagombea uchaguzi hawakubali kushindwa kwa kisingizio cha kuibiwa kura na hapo huwa ni mwanzo wa machafuko ya kisiasa. Wanasiasa hawana budi kujenga utamaduni wa kukubali matokeo, ikiwa kama uchaguzi umefanyika katika mazingira ya ukweli na uwazi. Pale wanapotia shaka, basi wafuate sheria na kanuni za nchi, ili haki iweze kutendeka.

Viongozi wa kisiasa wanapaswa kuungwa mkono na Jumuiya ya Kimataifa, lakini pia wawe na washauri makini kutoka ndani, watakaosaidia mchakato wa ujenzi wa Burkina Faso inayojikita katika misingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Baraza la Maaskofu linabainisha kwamba, halikuunga mkono mchakato wa kutaka kupindisha Katiba, ili kumruhusu Bwana Blaise Compaorè kuwania madaraka katika awamu ya tatu. Wanasiasa wajifunze kuheshimu Katiba ya Nchi.







All the contents on this site are copyrighted ©.