2015-01-21 07:36:25

Papa Francisko chemchemi ya matumaini na furaha!


Kardinali Oswald Gracias, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia anasema, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu nchini Ufilippini, imewakirimia wananchi matumaini mapya na furaha, baada ya kukabiliana na majanga, yaliyosababisha uchungu na majonzi mengi. Uwepo wa Baba Mtakatifu nchini Ufilippini, limekuwa ni tukio la furaha kuu, ambalo limewasaidia waamini kutambua tena umuhimu wa wao kujikita katika tunu msingi za maisha ya Kiinjili.

Itakumbukwa kwamba, Kardinali Gracias ni kati ya wale Makardinali wanane walioteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko, ili kumpatia ushauri wa kina katika mchakato wa mageuzi katika Sekretarieti ya Vatican kama yalivyoamriwa na vikao vya Makardinali. Anasema, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kutoa kipaumbele cha pekee kwa Bara la Asia, kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika majadiliano ya kidini na kitamaduni, ili Injili ya Kristo isaidie kujenga na kuimarisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu.

Baba Mtakatifu Francisko nchini Ufilippini amewaonjesha upendo na wao wakajibu kwa upendo pasi na unafiki, kiasi cha kuwashangaza walimwengu, watu millioni saba, walipojitokeza mjini Manila kwa ajili ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na Papa Francisko, siku ya mwisho ya hija yake ya kitume mjini Manila. Ujumbe wa Baba Mtakatifu kwa Familia ya Mungu nchini Ufilippini, umegusa undani wa maisha yao na kwamba, Injili ya Kristo ni msingi thabiti wa maisha, changamoto ya kuhakikisha kwamba, imani inamwilishwa katika matendo kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa watu.

Kwa upande wake Kardinali Orlando Quevedo kutoka Ufilippini anasema, changamoto ya kiimani iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa Familia ya Mungu nchini Ufilippini, itakuwa ni chachu ya kukoleza imani katika matendo, hasa wakati huu wananchi wengi wa Ufilippini wanapojitahidi kunyanyuka tena kutoka katika janga la Yolanda, lililowagusa na kuwatikisa hata katika imani yao.

Baba Mtakatifu amependa kuonesha upendo na mshikamano kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ndiyo maana, kulikuwa na ujumbe mkubwa wa wahanga wa dhoruba ya Yolanda,ambao walikutana wakazungumza na hatimaye, kupata chakula cha mchana na Baba Mtakatifu Francisko, tukio ambalo limeacha chapa ya kudumu katika mioyo ya maskini wengi. Hiki ni kielelezo cha mshikamano wa upendo kati ya Kanisa la Kiulimwengu na Kanisa mahalia.

Uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko nchini Ufilippini, umekuwa ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko makubwa; wameonja upendo na huruma yake; wakaguswa na unyenyekevu na upendo unaobubujika kutoka katika undani wa maisha. Ameishukuru na kuipongeza Serikali ya Ufilippini kwa kuanzisha mchakato wa haki, amani na upatanisho Kusini mwa nchi hiyo, kwa kuheshimu pia uhuru wa kuabudu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.